
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, ameliambia shirika la Habari la AFP kwamba ataitisha maandamano ikiwa Rais Yoweri Museveni ataupora uchaguzi mkuu utakaofanyika Alhamisi wiki hii, na kwamba atakaribisha uingiliaji kati wa Marekani.
Zaidi ya watu milioni 20 wamesajiliwa kupiga kura hiyo, ambapo Museveni mwenye umri wa miaka 81 ambaye ameitawala Uganda kwa miongo minne anatarajia kurefusha utawala wake kwa muhula mwingine.
Mpinzani mkuu wa Museveni, Bobi Wine mwenye umri wa miaka 43, atawania urais mara ya pili. Aliwania urais kwa mara ya kwanza mnamo 2021 ambapo alishindwa huku kukiwa na madai ya udanganyifu.
Kampeni zake zimekuwa zikikabiliwa na ukandamizaji mkali kutoka kwa vyombo vya usalama.