Kufikia sasa, Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte amekuwa akilinyamazia suala hilo ila mkakati huo hautaleta tija.
Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen ametahadharisha mwanzoni mwa wiki kuwa iwapo Marekani itaamua kuivamia kijeshi nchi mwanachama wa muungano huo wa kijeshi, kila kitu kitafikia kikomo. Kwa mantiki hiyo, Jumuiya na operesheni zake zote za usalama zilizozinduliwa mwishoni mwa Vita Vikuu ya Pili vya Dunia zitasitishwa.
Athari za vitisho na kauli hizo kwa NATO hazitakiwi kupuuzwa
Kwa mtazamo Patrick Oksanen, mchambuzi wa Shirika la Utafiti la Stockholm Free World Forum, hali iliyopo kwenye NATO kwa sasa ni ushindi kwa Urusi. Hii ni kwa sababu kauli na vitisho vinatolewa wakati ambapo umepita muda mfupi baada ya Marekani kuivamia Venezuela na pia mshauri wa rais Trump, Stephen Miller, kuhoji uhalali wa Denmark kuwa msimamizi wa Greenland na iwapo vikosi vyovyote vya bara la Ulaya vitaidhibiti Marekani.
Kulingana na Ed Arnold aliyezungumza na DW, kitendo cha Jumuiya hiyo kukaa kwenye meza ya mazungumzo kujadili kitisho kutoka kwa mmoja ya nchi wanachama kinatoa picha mbaya.
Kwa mtazamo wa baadhi ya wachambuzi, pendekezo moja ni washirika wa NATO kupeleka vikosi vyao Greenland, kumpa ishara Rais Trump kuwa suala la ulinzi wanalipa uzito mkubwa na kwamba hahitajiki kuchukua hatua hiyo.
Ulaya yaonywa juu ya usalama wa eneo la Arctic
Kwa upande wake, Steven Everts, mkurugenzi katika Taasisi ya Usalama ya Umoja wa Ulaya, mataifa ya Ulaya yanapaswa kulichukulia suala la usalama wa eneo la Arctic kwa uzito mkubwa na iwapo yapo mapungufu yaweze kufanyiwa kazi.
Mbunge wa Denmark katika Bunge la Umoja wa Ulaya Anders Vistisen, anaafiki mtazamo wa Steve Everts na kusisitiza kuwa ipo haja ya kuwa wakweli na kusitisha michezo ya kidiplomasia au kujaribu kuirai Marekani kutumia hekima na busara kadhalika kutenga hela zaidi kwa ulinzi wa kijeshi.
Kimsingi inachotaka Marekani hakiwezekani. Pendekezo jengine kutoka kwa wachambuzi wa Ulaya, ni kusitisha mkataba wa biashara kati ya Marekani na Ulaya ambao unatazamwa kuwa unaipendelea, hadi pale Washington itakapokomesha vitisho vya kutaka kuimiliki Greenland.
Kwenye kikao cha Paris cha kuiunga mkono Ukraine siku ya Jumanne, viongozi wa Ujerumani, Italia, Poland, Uhispania na Uingereza wailiunga mkono taarifa ya Waziri Mkuu wa Denmark Frederiksen na kwa pamoja kusisitiza kuwa walio na wajibu wa kulifanyia kazi suala hilo ni Denmark na Greenland pekee.
Taarifa hiyo ilitolewa muda mfupi kabla ya kikao na wawakilishi wa Marekani Steve Witkoff na Jared Kushner ambaye ni mkwe wa Rais Donald Trump, bila ya kuchelea athari ambazo zinaweza kutokea ukizingatia juhudi za Marekani za kuiunga mkono Ulaya kwenye suala zima la Ukraine.
