Rais Donald Trump wa Marekani alisema Jumanne kwamba anafuta matarajio ya mazungumzo na maafisa wa Iran huku kukiwa na msako mkali na ukandamizaji wa maandamano, akiwaambia raia wa Iran “msaada uko njiani unakuja.”
Trump hakutoa maelezo yoyote kuhusu kile ambacho msaada huo ungehusisha, lakini kauli yake inakuja baada ya siku chache zilizopita kusema Iran inataka kujadiliana na Marekani baada ya tishio lake la kuishambulia Jamhuri hiyo ya Kiislamu, ambapo idadi ya vifo kutokana na maandamano ya kitaifa imeongezeka hadi zaidi ya 2,000, kulingana na wachunguzi wa haki za binadamu.
Lakini Trump, akiwa na ujumbe wake wa hivi punde kwenye mitandao ya kijamii, alionekana kufanya mabadiliko ya ghafla kuhusu nia yake ya kushirikiana na serikali ya Iran. Trump aliandika katika chapisho la asubuhi kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social akisema “Wazalendo wa Iran, endeleeni kuandamana – dhbitini taasisi zenu!” “Hifadhi majina ya wauaji na wanyanyasaji. Watalipa gharama kubwa. Nimefuta mikutano yote na maafisa wa Iran hadi mauaji ya kipuuzi ya waandamanaji yakome. Msaada upo njiani.
Iran yamtuhumu Trump kwa kuchochea uvunjifu wa uthabiti wa kisiasa na vurugu
Iran imemtuhumu rais Trump Jumanne kwa kuchochea uvunjifu wa uthabiti wa kisiasa, kuchochea vurugu, na kutishia uhuru wa nchi, uadilifu wa eneo, na usalama wa taifa.
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa Amir Saeid Iravani aliandika katika barua yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akisema “Marekani na utawala wa Israeli zinabeba dhamana ya kisheria ya moja kwa moja na isiyopingika kwa vifo vya raia wasio na hatia, hasa miongoni mwa vijana.
Barua hiyo ambayo pia ilitumwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, aliiliandika kujibu chapisho la mitandao ya kijamii la Trump mapema Jumanne.
Trump aitaka Iran kuwaonyesha waandamanaji ubinadamu
Trump ameutolea wito utawala wa mjini Tehran kuwaonyesha ubinadamu waandamanaji huku kukiwa na ripoti za kuongezeka kwa idadi ya vifo katika ukandamizaji wa maandamano.
Trump alikuwa akishauriana na timu yake ya usalama wa taifa Jumanne kuhusu hatua zinazofuata kwa Iran huku akitafuta kuelewa vyema idadi ya raia wa Iran waliouawa na kukamatwa katika zaidi ya wiki mbili za machafuko kote nchini.
Trump alisema anaamini kwamba mauaji hayo ni “muhimu” na kwamba utawala wake “utachukua hatua ipasavyo.” Aliongeza kuwa anaamini serikali ya Iran ilikuwa “inafanya tabia mbaya.”
Lakini alisema bado hajapokea idadi iliyothibitishwa ya Wairan waliouawa katika maandamano yaliyoanza mwishoni mwa mwezi uliopita, akisema amesikia takwimu tano tofauti za idadi ya vifo.
Tangu maandamano yalipoanza Desemba 28, watu 16,700 wamekamatwa na zaidi ya 2,000 wameuawa, idadi kubwa ya waandamanaji, kulingana na Shirika la Habari la Wanaharakati wa Haki za Binadamu. Shirika hilo linategemea mtandao wa wanaharakati ndani ya Iran ambao unathibitisha vifo vyote vilivyoripotiwa.
Trump aonya kuhusu ‘hatua kali sana’ ikiwa Iran itawanyonga waandamanaji
Rais wa Marekani Donald Trump alionya Jumanne kuhusu “hatua kali sana” ambazo hazijatajwa dhidi ya Iran ikiwa mamlaka yake itaendelea na tishio la kuwanyonga baadhi ya waandamanaji, huku hasira za kimataifa zikiongezeka kuhusu msako ambao kundi moja la haki za binadamu lilisema huenda umewaua maelfu.
Vikundi vya haki za binadamu vinaishutumu serikali kwa kuwapiga risasi waandamanaji na kuficha ukubwa wa msako huo kwa kuzima mtandao ambao sasa umezidi alama ya siku tano.
Trump aliambia CBS News kwamba Marekani itachukua hatua ikiwa Iran itaanza kuwanyonga waandamanaji, baada ya waendesha mashtaka wa Tehran kusema mamlaka ya Iran itawasilisha mashtaka ya kifo ya “moharebeh”, au “kupigana vita dhidi ya Mungu”, dhidi ya baadhi ya washukiwa waliokamatwa kutokana na maandamano ya hivi karibuni.
Marekani yawataka raia wake kuondoka Iran
Marekani imewasihi raia wake kuondoka Iran mara moja, na kuwashauri kufikiria kuondoka kwa njia ya ardhi kwenda Uturuki au Armenia, kulingana na taarifa iliyotolewa Jumanne na ubalozi wa Marekani mtandaoni huko Tehran.
“Raia wa Marekani wanapaswa kuondoka Iran sasa. Fikiria kuondoka Iran kwa njia ya ardhi kwenda Uturuki au Armenia, ikiwa ni salama kufanya hivyo,” taarifa hiyo ilisema.
