Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam yatambuliwa kuwa hospitali binafsi bora zaidi Tanzania katika Tuzo za Health Africa 2025Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam yatambuliwa kuwa hospitali binafsi bora zaidi Tanzania katika Tuzo za Health Africa 2025

Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam imetambuliwa kama Hospitali Binafsi Bora Zaidi Tanzania katika Tuzo za Health Africa 2025 zilizoandaliwa na Health Africa Events na kufanyika Desemba 15, 2025. Hafla hiyo ililenga kutambua taasisi zilizoonyesha dhamira endelevu katika kuboresha huduma za afya na kuimarisha mifumo ya afya barani Afrika.

Hafla ya tuzo hizo iliwakutanisha viongozi wa sekta ya afya, watunga sera na taasisi mbalimbali ambazo mchango wao umeleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma za afya, uimara wa mifumo ya afya na upatikanaji wa huduma bora barani Afrika ikiongozwa na kaulimbiu isemayo: “Kuimarisha mifumo ya afya kwa ajili ya huduma ya afya kwa wote kupitia ushirikiano, ubunifu, na usawa.”

Tuzo hii inaakisi msisitizo endelevu wa Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam katika kutoa huduma salama, zenye uhakika na zinazomlenga mgonjwa, sambamba na mchango wake katika kuendeleza mifumo ya afya nchini Tanzania. Kwa zaidi ya miaka 96, Huduma za Afya za Aga Khan Tanzania zimekuwa zikisaidia kuimarisha mifumo ya kitaifa ya afya na kupanua upatikanaji wa huduma salama na zenye ubora wa hali ya juu kwa jamii mbalimbali nchini.

Katika kipindi chote hicho, hospitali hiyo imeendelea kutambuliwa kitaifa na kimataifa katika maeneo muhimu kama vile ubora wa huduma za kitabibu, uongozi na usimamizi bora, kinga dhidi ya maambukizi, ubora wa huduma kwa wateja, ubunifu na miradi ya afya inayolenga jamii.

Kwa sasa, Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam bado ndiyo hospitali pekee nchini iliyopata ithibati ya kimataifa kutoka Joint Commission International (JCI), Marekani na imepata Muhuri wa Dhahabu wa Uidhinishaji (Gold Seal of Approval) kwa mara ya nne mwaka 2025.

Hospitali hiyo pia imepata tuzo mbalimbali kutokana na mchango wake katika utoaji wa huduma za kitaalamu, zikiwemo: Tuzo ya Kimataifa ya Ubora wa Huduma (International Service Excellence Award) kutoka Taasisi ya Usimamizi wa Wateja (CICM) Machi 28, 2025, Tuzo ya Huduma Bora za Maabara kutoka Randox International Quality Assessment Scheme (RIQAS) Septemba 20, 2025.

Tuzo ya Hospitali Bora Binafsi Tanzania ambayo Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam imeshinda katika Tuzo za Health Africa 2025, zilizofanyika Desemba 15, 2025 jijini Dar es Salaam.

Tuzo ya Ubora katika Utoaji wa Huduma za Kupambana na Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa (Anti-Microbial Resistance Champion Award) iliyotolewa katika Mkutano wa saba wa Kisayansi barani Afrika wa WAAW Desemba 3, 2025, Tuzo ya Uwasilishaji Bora wa Taarifa za Fedha kutoka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania Desemba 4, 2025 na ithibati kadhaa za kimataifa za huduma za maabara kutoka SADCAS (ISO 15189:2022) na Usalama wa Chakula FSMS (ISO 22000).

Tuzo nyingine muhimu za kimataifa ambazo Hospitali ya Aga Khan imeshinda ni Tuzo ya Shaba (Bronze Award) ya uongozi na usimamizi katika kuboresha huduma za saratani nchini na kutambuliwa kwa mchango wa hospitali hiyo katika uwajibikaji wa kijamii na kimazingira kupitia kuboresha maisha ya waathirika wa moto na ukatili kwa kuwawezesha kupata huduma za upasuaji wa kurekebisha maumbile. Tuzo hizi zimetolewa Novemba 12, 2025 na Shirikisho la Kimataifa la Hospitali (IHF) katika Mkutano wa 48 wa Hospitali Duniani uliofanyika Geneva, Uswisi.

Kwa pamoja, jitihada hizi zinaakisi mtazamo wa kina katika utoaji wa huduma za afya, unaochanganya viwango vya kimataifa na mahitaji ya ndani pamoja na ubora wa kitabibu unaoendana na huduma, kujifunza na ushirikiano.

Kwa mawasiliano zaidi, tafadhali wasiliana na:

Geofrey Anael

Mratibu wa Mawasiliano ya Umma

Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam

📞 +255 654 540 226

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *