Hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 huko Morocco imewadia katika wakati ambao kila mtu anaongea lake kuhusu mechi hizo za kibabe ambazo zinawakutanisha majina makubwa ambayo yamekuwa yakitamba katika soka la ushindani barani Ulaya.
Baada ya wiki kadhaa kushuhudia soka la kiwango cha juu katika hatua makundi, 16 bora na robo fainali, sasa ni mataifa manne pekee yaliyosalia kwenye mbio za kuwania taji la Afrika ambayo ni Nigeria, Morocco, Senegal na Misri, kila moja likibeba historia, fahari na matarajio makubwa kutoka kwa mamilioni ya mashabiki wao.
AFCON ya mwaka huu imeonesha wazi mabadiliko ya soka la Afrika. Timu zimewasili zikiwa zimejiandaa vilivyo kuanzia kiufundi na kimbinu. Hakuna tena dhana ya timu ndogo au kubwa katika hatua za mwisho, bali ni nani aliyejiandaa vizuri zaidi na mwenye nidhamu ya kifundi na aliye tayari kukabiliana na presha ya ushindani.
Mechi za nusu fainali ambazo zinapigwa leo, Jumatano katika viwanja viwili tofauti ni mtihani wa mwisho kabla ya fainali na mara nyingi huamua sio tu nani anaingia fainali, bali pia nani wa kuweka historia ya kukumbukwa.
Kwa wenyeji Morocco, hii ni nafasi ya kipekee ya kuandika historia mbele ya mashabiki wao. Kwa Nigeria, ni safari ya kulipa kisasi cha maumivu ya kukosa tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2026.
Senegal wanatafuta kurejesha hadhi yao kama wafalme wa soka la Afrika, huku Misri wakisaka kuongeza nyota ya nane (tayari wanasaba kufuatia kutwaa taji hilo kwa idadi hiyo), kwenye jezi zao.
NIGERIA vs MOROCCO
Nusu fainali ya kwanza ya AFCON 2025 itawakutanisha Nigeria na wenyeji Morocco katika Uwanja wa Prince Moulay Abdellah mjini Rabat. Huu ni mchezo unaobeba uzito mkubwa wa kihistoria na kiufundi huku kila upande ukiingia ukiwa na falsafa tofauti kabisa ya soka.
Nigeria wamekuwa moja ya timu zinazovutia zaidi katika mashindano haya. Walifika AFCON wakiwa na maumivu baada ya kushindwa kufuzu Kombe la Dunia 2026, tukio lililotikisa Nigeria. Badala ya kusambaratika, Super Eagles wamegeuza maumivu hayo kuwa hasira kali uwanjani dhidi ya kila mpinzani anayekatisha mbele yao chini ya kocha Eric Chelle.
Safari yao imekuwa ya kushangaza tangu mwanzo wa mashindano. Ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania ulionesha uwezo wao wa kushambulia, lakini ushindi wa 3-2 dhidi ya Tunisia ulithibitisha tabia yao ya kupambana hadi mwisho. Katika mchezo wa mwisho wa makundi, Nigeria waliwapa nafasi wachezaji wengine kabisa lakini bado wakaibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Uganda.
Hatua ya mtoano imeonyesha wao ni taifa la namna gani na nini wanahitaji katika mashindano hayo. Ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Msumbiji katika raundi ya 16 ulionesha ukatili wao mbele ya lango. Robo fainali dhidi ya Algeria ilikuwa mtihani halisi, lakini Super Eagles walionyesha ukomavu mkubwa kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa katika mashindano hayo.
Nigeria kwa sasa ndio vinara wa ufungaji katika AFCON 2025 wakiwa na mabao 14 katika mechi tano. Victor Osimhen amekuwa mfano wa mshambuliaji wa kisasa kutokana na nguvu, kasi, kujituma na uwezo wa kumalizia nafasi kwa ufanisi mkubwa. Ademola Lookman ameongeza kasi na ubunifu upande wa pembeni, huku Alex Iwobi akiwa kiungo muhimu kinachounganisha safu ya kati na ushambuliaji.
Changamoto kubwa kwa Nigeria ni kukosekana kwa nahodha Wilfred Ndidi, ambaye atakosekana katika mchezo huu kutokana na adhabu ya kadi. Hata hivyo, uwepo wa Raphael Onyedika na Frank Onyeka unatarajiwa kudumisha uwiano wa kiungo. Safu ya ulinzi inayojumuisha Calvin Bassey na Semi Ajayi imeonesha ubora wa aina yake, huku kipa Stanley Nwabali akijijengea sifa kama mmoja wa makipa bora wa mashindano.
Kwa upande wa Morocco, nguvu yao kubwa imekuwa kwenye ulinzi na nidhamu ya kiufundi. Chini ya kocha Walid Regragui, Atlas Lions wamejenga timu inayocheza kwa mpangilio na matumizi sahihi ya nafasi.
Morocco wameruhusu bao moja pekee katika mashindano yote na hakuna bao lililofungwa dhidi yao kwa mashambulizi ya kawaida yani ‘open play’ kwa Kiingereza, jambo linaloonesha uimara wao.
Brahim Diaz amekuwa nyota wa mashindano kwa upande wa Morocco, akifunga katika mechi tano mfululizo rekodi adimu katika AFCON. Achraf Hakimi ameongeza kasi na uzoefu upande wa kulia, huku kipa Bono akiwa ngome imara langoni. Historia kati ya wababe hawa, inaipa Morocco faida kidogo, hasa katika miaka ya karibuni, lakini Nigeria wanaonekana kuwa na makali zaidi katika ushambuliaji.
Nigeria: Nwabali; Osayi-Samuel, Ajayi, Bassey, Onyemaechi; Onyeka, Onyedika, Iwobi; Lookman, Akor Adams, Osimhen
Morocco: Bono; Hakimi, Aguerd, Masina, Mazraoui; El Khannouss, El Aynaoui, Saibari; Brahim Diaz, Ezzalzouli, El Kaabi
Uzoefu, Historia
Nusu fainali ya pili itawakutanisha Senegal dhidi ya Misri katika mchezo unaotarajiwa kujaa tahadhari kubwa za kiufundi. Hii ni mechi ya mataifa mawili yenye uzoefu mkubwa wa hatua za juu za AFCON na kila upande unaingia ukiwa na silaha zake muhimu.
Senegal wameonekana kuwa timu iliyokamilika zaidi katika mashindano haya. Wakiwa na uwiano mzuri kati ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji, Simba hao wa Teranga wamefunga mabao 11 katika mechi tano na kuruhusu mabao mawili pekee.
Chini ya kocha Pape Thiaw, Senegal waliiondoa Sudan kwa ushindi wa 3-1 katika raundi ya 16, kabla ya kuifunga Mali 1-0 katika robo fainali. Sadio Mane amekuwa nahodha wa mfano, akitoa pasi za mwisho tatu na kuongoza timu kwa uzoefu na utulivu. Iliman Ndiaye na Nicolas Jackson wameongeza makali katika safu ya ushambuliaji, huku Pape Gueye akiwa mhimili wa kiungo.
Misri, kwa upande wao, wamepitia njia yenye misukosuko zaidi. Ushindi wao mwingi umekuja kwa tabu, wakihitaji mabao ya dakika za mwisho, penalti au muda wa nyongeza. Hata hivyo, uzoefu wao katika mechi kubwa ni kitu cha kutazamwa. Ni mabingwa mara saba wa AFCON.
Mohamed Salah amekuwa tegemeo kuu la Pharaohs. Akiwa na mabao manne, yuko katika mbio za Kiatu cha Dhahabu na pia anawinda rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Misri katika AFCON. Omar Marmoush na Trezeguet wamekuwa wakijaribu kumpa msaada, huku safu ya ulinzi ikionyesha mapungufu yanayoweza kutumiwa na Senegal.
VIikosi vinavyoanza
Senegal: Mendy; Diatta, Koulibaly, Niakhate, Diouf; Diarra, Idrissa Gueye, Pape Gueye; Ndiaye, Nicolas Jackson, Sadio Mane
Misri: El Shenawy; Hany, Ibrahim, Rabia, Fatouh; Attia, Fathi, Adel; Salah, Marmoush, Trezeguet.
