
Bagamoyo, wilaya hii iko mkoa wa Pwani, Mashariki mwa Tanzania eneo la Afrika Mashariki. Bwana Venance anaeleza jinsi ugonjwa wa homa ya bonde la ufa unavyoenezwa.
“Eneo letu lina idadi kubwa ya mifugo, ikiwemo takribani ng’ombe 57,000, mbuzi 15,000 na kondoo 3,700. Homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever – RVF) ni ugonjwa wa virusi unaoenezwa zaidi na mbu wa jamii ya Culex na Aedes.”
Tanzania inatumia mbinu iitwayo Rift Valley Fever DST kufuatilia maeneo hatarishi ya milipuko ya RVF. Dioniz Ibrahim ambaye ni, Afisa wa Mifugo, Wizara ya Mifugo, nchini humo anaeleza.
“Zana ya Rift Valley Fever DST pia inasaidia kile tunachokiita ufuatiliaji unaozingatia hatari . Kama mnavyojua, tuna eneo la nchi yetu ni kubwa na rasilimali chache. Hivyo, kwa kuwa DST inaonesha maeneo ya kijiografia yenye hatari kubwa ya maambukizi, itasaidia wizara pamoja na Kurugenzi ya Huduma za Mifugo kujua ni wapi pa kuzingatia ufuatiliaji, kwa kuzingatia sayansi na ushahidi unaotolewa na zana hii.”
Je ni kwa vipi onyo la mapema lina faida? Bwana Venance anarejea kuelezea.
“Onyo la mapema linatuwezesha kuwasiliana na kuchukua hatua za haraka. Tunapojua RVF ina uwezekano wa kujitokeza, tunaweza kuwajulisha maafisa wa mifugo na kuwaelimisha wafugaji. Hatua rahisi kama kukausha mashimo yenye maji na kunyunyizia viuatilifu katika vinamasi zinaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya kuenea kwa ugonjwa.”
Claudia Pitiglio, Mtaalamu Mwandamizi wa Ikolojia ya Magonjwa, FAO, anasema:
“Tumebaini na kushuhudia kwamba pale ambapo mbinu hii imetumika, kumekuwepo na uwezekano wa kufuatilia hali halisi kwenye maeneo husika, na hivyo kuwa na mwitikio wa haraka zaidi katika kutambua hatua za awali za Homa ya Bonde la Ufa (RVF). Hali hii imewawezesha kutekeleza ufuatiliaji unaozingatia hatari na kugawa rasilimali katika maeneo ambayo yako hatarini zaidi. Hili ni jambo muhimu sana.”
FAO inasema kwa kutumia zana hii ya RVF DST, Tanzania inaimarisha mfumo wa Afya Moja (One Health) unaojumuisha mifugo, binadamu, na mazingira. Ufanisi wake unaonesha jinsi teknolojia na maarifa ya kisayansi yanavyoweza kusaidia nchi kuzuia milipuko ya magonjwa hatari na kulinda ustawi wa wananchi wake.
