
Kwa mujibu wa uchambuzi wa WMO wa seti nane za kimataifa za takwimu za halijoto, wastani wa halijoto ya uso wa dunia mwaka 2025 ulikuwa nyuzi joto 1.44°C juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda.Hii iliufanya mwaka huo kushika nafasi ya pili au ya tatu kati ya miaka 176 ya rekodi za hali ya hewa.
Muhimu zaidi uchambuzi huo umesema , miaka 11 iliyopita kuanzia 2015 hadi 2025 sasa ndiyo miaka 11 yenye joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa.
Katibu Mkuu wa WMO, Celeste Saulo amesema “Mwaka 2025 ulianza na kuhitimishwa na hali ya kupoa ya La Niña, lakini bado ulikuwa miongoni mwa miaka yenye joto kali zaidi duniani. Hii ni kwa sababu ya mkusanyiko wa gesi chafu zinazohifadhi joto katika angahewa yetu.”
La Niña haikuzuia mwelekeo wa joto la muda mrefu
Kipindi cha miaka mitatu kati ya 2023 na 2025 kilikuwa cha joto zaidi kuwahi kupimwa, kikiwa na wastani wa nyuzi joto 1.48°C juu ya kiwango cha 1850–1900.
Wanasayansi wanasema hali hii inathibitisha kuwa mabadiliko ya muda mfupi ya tabianchi, kama La Niña, hayawezi tena kufidia mwelekeo wa ongezeko la joto unaochochewa na shughuli za binadamu.
Halijoto ya juu ya ardhi na bahari mwaka 2025 ilichangia kutokea kwa matukio makubwa ya mabadiliko ya tabianchi yakiwemo mawimbi ya joto, mvua kubwa na vimbunga vya kitropiki vyenye nguvu.
“Hali hizi zinaonesha umuhimu mkubwa wa mifumo ya tahadhari ya mapema,” amesisitiza Saulo.
Bahari zinaendelea kufyonza joto
Utafiti mwingine uliotajwa na WMO unaonesha kuwa joto la bahari lilifikia viwango vya juu karibu na kuvu nja rekodi mwaka 2025, likidhihirisha uhifadhi wa muda mrefu wa joto la ziada katika mfumo wa tabianchi.
Takribani asilimia 90 ya joto linalotokana na ongezeko la joto duniani huhifadhiwa katika bahari, na kuifanya halijoto ya bahari kuwa kiashiria muhimu cha mabadiliko ya tabianchi.
Kuanzia 2024 hadi 2025, mita 2,000 za juu za bahari duniani ziliongezeka kwa takribani zettajouli 23 za joto sawa na takribani mara 200 ya jumla ya uzalishaji wa umeme duniani kwa mwaka mmoja.
Zaidi ya nusu ya eneo la bahari duniani liliingia katika miaka mitano yenye joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa, ikijumuisha Bahari ya Atlantiki, Hindi na Kusini, pamoja na Bahari ya Mediterania.
Tathmini moja ya kuaminika ya halijoto ya dunia
Kwa mara ya kwanza, WMO imeunganisha seti nane za kimataifa za takwimu zikiwemo kutoka NASA, NOAA, Copernicus, Ofisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza, Japan na China ili kutoa tathmini moja ya kuaminika ya halijoto ya dunia.
“Taarifa za Dunia zilizo sahihi, zinazopatikana kwa urahisi na zinazoweza kutekelezwa ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote,” amesema Saulo akiongeza kuwa “Ushirikiano huu wa kisayansi unaweka msingi wa maamuzi bora duniani kote.”
WMO itachapisha ripoti kamili ya Hali ya Tabianchi Duniani 2025 mwezi Machi 2026, ikieleza kwa kina mwelekeo wa halijoto pamoja na viwango vya gesi chafu, kupanda kwa kina cha bahari, kuyeyuka kwa barafu na athari za matukio makubwa ya hali mbaya ya hewa.
