Akizungumza na wajumbe wa Baaraza hilo jijini New York Marekani, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Hans Grundberg, amesema matukio ya kisiasa na usalama ya hivi karibuni hasa kusini mwa nchi hiyo yanaonesha jinsi utulivu unavyoweza kudhoofika haraka bila mchakato wa kisiasa unaoaminika na unaojumuisha pande zote.
“Bila mbinu ya kina inayoshughulikia changamoto nyingi za Yemen kwa njia ya pamoja badala ya kipekee, hatari ya mizunguko ya ukosefu wa utulivu itabaki,” amesema Bwana Grundberg.
Hans Grundberg (kwenye skrini), Mjumbe wa Maalum wa Katibu Mkuu kwa ajili ya Yemen, akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali nchini Yemen.
Mizozo Kusini mwa nchi
Ingawa kupungua kwa mvutano wa kijeshi kumefanikishwa katika siku za karibuni, ameonya kwamba hali ya usalama bado ni dhaifu, hasa kufuatia kupelekwa kwa nguvu za pande zinazozozana katika mikoa ya kusini.
Mwezi Desemba, vikosi vinavyohusiana na Halmashauri ya Mpito ya Kusini vilijaribu kupanua uwepo wao katika maebeo ya Hadramout na Al Mahra, huku vikosi vinavyoungwa mkono na serikali, vilivyoungwa mkono na Saudi Arabia, vikichukua hatua mapema Januari kudhibiti miundombinu muhimu.
Bwana Grundberg amesema “mustakabali wa kusini mwa Yemen hauwezi kuamuliwa na mhusika mmoja pekee au kwa kutumia nguvu,” akihimiza viongozi wa Yemen kufuata mazungumzo.
Alikumbatia pendekezo la Rais Rashad al-Alimi la kuandaa mazungumzo na viongozi mbalimbali wa kusini, amesema ni hatua inayoweza kupelekea ujenzi upya wa mchakato wa kisiasa wa Yemen chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.
Miaka ya migogoro imewaacha maelfu ya Weyemen wakiwategemea misaada ya kibinadamu.
Ukosefu wa utulivu unadhuru uchumi
Kutokuwepo utulivu wa kisiasa kunahisiwa zaidi katika uchumi wa Yemen, aamesema, huku bei zikiongezeka, mishahara kutolipwa na huduma kudorora, hivyo kudhoofisha uwezo wa kaya.
“Hata ukosefu wa utulivu wa kisiasa na usalama kwa muda mfupi unaweza kusababisha shinikizo la sarafu, kupanua pengo la kifedha, na kuchelewesha juhudi za mageuzi,” alionya Bwana Grundberg.
Mizigo ya kiuchumi inazidiwa na taasisi dhaifu na malipo yasiyo ya kawaida ya mishahara, hasa kwa wafanyakazi wa sekta ya umma.
Bwana Grundberg amehimiza mamlaka za Yemen kulinda taasisi za kiuchumi ikiwemo Benki Kuu dhidi ya migongano ya kisiasa, akionya kwamba kupotea kwa imani kunaweza kudhoofisha nchi zaidi.
Ramesh Rajasingham (kwenye skrini), Mkurugenzi wa Idara ya Sekta ya Kibinadamu na Mkuu na Mwakilishi wa Ofisi ya Uratibu wa Mambo ya Kibinadamu huko Geneva (OCHA), akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali nchini Yemen.
Madhara makubwa ya kibinadamu
Ramesh Rajasingham, Mkurugenzi wa Sekta ya Kibinadamu katika ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya Kibinadamu na Masuala ya Dharura OCHA, amesema mgogoro wa Yemen unaongezeka huku mahitaji yakiongezeka, na upatikanaji wa misaada umekua mgumu kutokana na uhaba wa fedha.
Zaidi ya Weyemen milioni 18 takriban nusu ya idadi ya watu wote watakabiliana na uhaba wa chakula mkali mwezi ujao, huku maelfu wakiweza kuingia kwenye hali ya njaa kubwa, wakikabiliwa na hali zinazofanana na njaa, ameonya.
Mfumo wa afya pia unadhoofika. Zaidi ya vituo 450 tayari vimefungwa na maelfu zaidi viko hatarini kupoteza ufadhili.
Programu za chanjo pia ziko hatarini na watoto wachache wa Yemen wameripotiwa kuchanjwa kikamilifu, hasa kutokana na upatikanaji mdogo eneo la kaskazini.
“Kwa matokeo hayo, mamilioni ya watoto wa Yemen wako hatarini kutokana na magonjwa hatari lakini yanayoweza kuzuiawa kwa chanjo, kama vile surua, diftheria, kipindupindu na polio,” amesema Bwana Rajasingham.
Vizuizi vya misaada
Operesheni za kibinadamu zinazidi kuwekewa vikwazo kutokana na kuendelea kushikiliwa kwa wafanyakazi 73 wa Umoja wa Mataifa na mamlaka za Houthi, amesema Bwana Rajasingham, akitaka kuachiwa kwao mara moja.
Ushikiliwaji wao umepunguza sana utoaji wa misaada katika maeneo yanayoishi kwa kuitegemea kwa takriban asilimia 70 ya mahitaji ya kibinadamu nchini kote.
Licha ya changamoto hizo, misaada inaendelea pale panapopatikana ufikiaji. Washirika wa Umoja wa Mataifa walifikia watu milioni 3.4 kwa msaada wa chakula mwishoni mwa mwaka jana na kutoa msaada wa dharura wakati wa mafuriko na milipuko ya magonjwa. Lakini mafanikio hayo ni dhaifu.
“Hatua za kibinadamu husaidia kuokoa maisha,” amesema Bwana Rajasingham, “lakini pale ufikiaji unapozuiwa na fedha kupungua, mafanikio hayo hurudiwa haraka.”
Shambulio Bahari ya Sham
Mapema leo Jumatano, Baraza la Usalama pia liliipitisha uamuzi wa kuongeza kwa miezi sita, mahitaji ya kuripoti kila mwezi kuhusu mashambulio ya kikundi chenye silaha cha Houthi ambacho kinadhibiti sehemu kubwa ya Yemen dhidi ya meli za kibiashara na biashara katika Bahari ya Sham.
Azimio hilo liliidhinishwa kwa kura 13 za ndiyo, huku Urusi na China wakijiweka pembeni.
Hali hiyo ilianzishwa Januari 2024 kufuatia ongezeko la mashambulio ya Houthi kwenye usafirishaji wa kimataifa unaohusiana na mgogoro wa Gaza.
Ilimpa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa jukumu la kutoa taarifa za mara kwa mara juu ya matukio ya usalama wa baharini, athari zake za kibinadamu na kiuchumi, na matokeo yake kwa utulivu wa kikanda.
