Dakar – AGRA, kwa ushirikiano na Mastercard Foundation, inaendesha mpango wa kuongeza kufadhili vijana kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo barani Afrika. Mpango huu, uliopewa jina Youth Entrepreneurship for the Future of Food and Agriculture, ni mradi wa miaka mitano unaolenga kufungua fursa za ajira kwa vijana kote barani.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa Nana Amoah, Mkurugenzi wa Jinsia wa AGRA, mpango huu unatekelezwa katika ngazi mbili. Kwanza, katika sera, AGRA inashirikiana na serikali, taasisi za kikanda na Umoja wa Afrika kuhakikisha sauti za vijana zinajumuishwa katika sera za kilimo kama vile Comprehensive Africa Agriculture Development Programme (CAADP). Pili, katika ngazi za jamii, Agra inashirikiana na kampuni binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi za kifedha ili kuboresha upatikanaji wa fedha, masoko na maendeleo ya ujuzi.

Amoah anasema kuwa, ukiwa katika mwaka wa pili, mpango huu tayari umefikia vijana zaidi ya milioni moja na kuunda nafasi zaidi ya 113,000 za ajira. AGRA inautekeleza mradi huu katika nchi saba: Rwanda, Malawi, Ghana, Tanzania, Burkina Faso, Msumbiji na Mali.

Kipaumbele kikubwa, kulingana na Amoah, kimekuwa kushughulikia changamoto kama vile ukosefu wa bidhaa za kifedha rafiki kwa vijana, mitazamo hasi kuhusu kilimo, na ukosefu wa uelewa kuhusu njia mbalimbali za kazi katika sekta ya chakula na kilimo.

Vijana wakulima Africa
Vijana wakulima Africa FLICK STUDIOS 2024

Aidha, Amoah anaeleza kuwa mpango huu unatoa mafunzo katika biashara ya kilimo, ujasiriamali, matumizi ya mitambo ya kisasa, umwagiliaji, usalama wa chakula na vyeti. Anasisitiza kuwa ujuzi huu ni muhimu katika kuwaandaa vijana kunufaika na fursa zilizopo kwenye shughuli za kilimo shambani na zisizo za shambani.

Miongoni mwa hadithi za mafanikio, Nana Amoah anataja mfano wa mfanyabiashara wa pembejeo za kilimo nchini Malawi ambaye, kwa msaada wa mpango huu, ameongeza biashara yake, kuanzisha mtandao wa warithi (franchise), na kuajiri vijana kumi zaidi. Hali kama hiyo pia imeripotiwa Rwanda, Msumbiji na Tanzania, ambapo vijana wanajiendeleza kupitia kilimo.

Tinga za kulima mashamba
Tinga za kulima mashamba FLICK STUDIOS 2024

Kwa mujibu wa Amoah, mpango huu unaakisi uhalisia wa kidemografia barani Afrika, ambapo idadi kubwa ya vijana ina uwezo wa kuunda mustakabali wa chakula na kilimo. Anasema kuwa kwa kuwekeza katika ubunifu na uongozi wa vijana, AGRA inalenga kulifanya kilimo kuwa kichocheo cha ukuaji jumuishi na usalama wa chakula barani Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *