Canada. Mwanamuziki wa Pop, Rock na R&B kutokea Canada, Celine Dion, 57, ameeleza kwa hisia kali jinsi anavyomkumbuka mumewe marehemu Rene Angelil, ikiwa ni miaka 10 tangu kifo chake.
Celine, mkali wa kibao maarufu cha Because You Loved Me (1996), amesema yeye pamoja na watoto wake bado wanamkumbuka sana Rene na wataendelea kumpenda daima.
Jumatano hii kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii aliposti picha ya Rene ikiwa juu ya piano kama ishara ya kuhadhimisha ya miaka 10 tangu alipofariki.
“Kipenzi changu, miaka 10 bila wewe nahisi kama ni siku moja tu, na bado kila siku nahisi kama muongo mmoja… Miaka 10 bila mguso wako, na bado kila siku nahisi mguso wako,” alieleza na kuongeza.
“Tunakukumbuka zaidi ya tunavyoweza kustahimili, lakini unatupa nguvu ya kuwa wahimilivu… Tunakupenda sana, kila siku na kila mwaka,” ujumbe wa Celine ulieleza.
Mume wa Celine, Rene alifariki akiwa na umri wa miaka 73 hapo Januari 14, 2016, zikiwa ni siku mbili kabla ya siku yake ya kuzaliwa. Sababu ya kifo chake ni saratani ya koo, ugonjwa aliogundulika nao mwaka 1999.
Wawili hao walifunga ndoa hapo Desemba 17, 1994 katika kanisa Kuu la Notre-Dame, Montreal, na walijaliwa kupata watoto watatu – Charles (2001) na pacha Nelson na Eddy (2010).
Kwa mara ya kwanza walikutana mwaka 1980, wakati huo Celine akiwa na umri wa miaka 12. Rene alivutiwa na kipaji chake na kujitolea kuwekeza na kuwa meneja wake hadi akaja kuwa mwanamuziki mkubwa.
Walifanya kazi pamoja kwa miaka saba kabla ya kuchumbiana mwaka 1987, wakati huo Celine akiwa na miaka 19, na alipofikisha miaka 25 ndipo wakafunga ndoa.
Mwaka uliopita katika siku ya kina baba duniani, Celine alitoa ujumbe kuhusu siku hiyo huku akieleza kile anachokumbuka kutoka kwa Rene kuhusu malezi ya watoto wao.
“Leo nawaza kuhusu kina baba wote wanaowalea watoto wao kwa upendo, subira, na nguvu wakijitahidi kuwa pamoja nao kila wakati. Asanteni kwa yote mnayoyafanya”.
“Kwa mpenzi wangu Rene… huenda haupo tena nasi kimwili, lakini upendo wako unaishi ndani yetu. Ulitufundisha kuwalea wavulana wetu kuwa wema, kujiamini, na kuthaminiana. Hiyo ndio zawadi kuu kuliko zote”.
“Na kwa baba yangu mpendwa, asante kwa upendo wako na uwepo wako wa kudumu katika maisha yangu. Ulinishangilia baada ya kila wimbo, ulikuwa shabiki yangu namba moja. Upo nami daima. Siku njema ya kina Baba,” alisema Celine.
Celine aliyevuma na ngoma, I’m Alive (2002) kutoka katika albamu yake ya saba, A New Day Has Come (2002), ameshinda tuzo sita za Grammy huku akishikilia rekodi kama msanii wa Kifaransa aliyeuza zaidi kwa wakati wote.