Dar es Salaam. Simba imemtambulisha kiungo mshambuliaji raia wa Senegal, Libasse Gueye kama mchezaji wake mpya baada ya kukamilisha usajili wake akitokea Teungueth ya Senegal.

Gueye (22), amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili na nusu ambao utafikia tamati Juni 2028.

Gueye anamudu kucheza nafasi tofauti uwanjani ambapo mbali na kiungo mshambuliaji pia anaweza kucheza kama winga.

Kiwango bora alichokionyesha katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) 2024 kimeonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kuishawishi Simba kumnasa nyota huyo.

Gueye ni mchezaji mwenye kasi na uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za mabao.

Gueye amesajiliwa kuziba nafasi ya Jean Charles Ahoua ambaye ameuzwa CR Belouizdad ya Algeria.

Kiungo huyo anakuwa mchezaji wa tatu raia wa Senegal kuitumikia Simba akifuata nyayo za Pape Ndaw na Pape Osmane Sakho.

Hapana shaka kibarua cha kwanza kwa Gueye kitakuwa ni mechi ya ugenini ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance ya Tunisia ambayo itachezwa Januari 24, 2026.

Simba inahitajika kupata ushindi katika mechi hiyo ili iweke hai matumaini yake ya kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo baada ya kupoteza mechi mbili za mwanzo dhidi ya Petro Luanda na Stade Malien.

Ilifungwa bao 1-0 nyumbani na Petro na mchezo uliofuata ikafungwa mabao 2-1 ugenini na Stade Malien.

Matokeo hayo yameifanya Simba iburute mkia katika kundi D ikiwa haina pointi hata moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *