
Iringa. Katika kuhakikisha watoto yatima wanakuwa kwa ustawi na kupata malezi bora, jamii mkoani Iringa imeombwa kuacha tabia ya kuwatelekeza mara baada ya kuwapeleka katika vituo vya kuwalea.
Wito huo umetolewa leo Jumamosi, Januari 17, 2026 na Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Iringa, Habiba Sanze, wakati wa kukabidhi msaada wa Serikali kwa watoto yatima waliopo katika Kituo cha Tosamaganga Home Centre kilichopo wilayani Iringa.
Sanze amesema changamoto kubwa inayokabili vituo vya kulelea watoto yatima ni kitendo cha ndugu au wazazi kuwapeleka vituoni na kisha kutowafuatilia tena.
“Tabia hiyo inawaathiri watoto kisaikolojia na kihisia, kwani hukosa faraja ya malezi ya kifamilia licha ya kupata huduma muhimu vituoni,” amesema Ofisa Sanze.
Amesisitiza kuwa kuwapeleka watoto katika vituo haimaanishi familia au jamii imemaliza wajibu wake, bado ina jukumu la kuendelea kuwajali na kushiriki katika malezi yao.
“Ushiriki wa familia ni muhimu katika ukuaji wa mtoto, hasa kwa yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu,” amesema.
Akizungumzia hali ya vituo wilayani Iringa, Sanze amesema wilaya hiyo ina makao manne ya kulelea watoto yatima, yakiwemo Kituo cha Tosamaganga Home Centre.
Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kusimamia na kutoa miongozo kwa vituo hivyo ili kuhakikisha watoto wanapata ulinzi, malezi bora, elimu na huduma za afya.
Akiwakilisha msaada huo kwa niaba ya Serikali, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ashery Mdalila, amesema jumla ya watoto 490 wamefikiwa na msaada huo.
Kwa upande wake, Sista Winfrida Mhongole kutoka Kituo cha Tosamaganga Home Centre, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa msaada kwa watoto yatima kila mwaka.