Waziri Mkuu wa Iraq amekosoa vikali unyama na mauaji ya kigaidi huko Ghaza na Lebanon, mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Israel nchini Syria, pamoja na tishio dhidi ya Iran ambayo ni nchi jirani na Iraq.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Iraq, Muhammad Shi’a Al-Sudani amesema hayo usiku wa kuamkia leo Jumapili katika sherehe ya Siku ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu nchini Iraq. Amesema: “Nchi za Kiislamu na Kiarabu zinakabiliwa na njama hatari zinazoshambulia uwepo wa nchi zao na itikadi zao za kidini.”

Al Sudani ameongeza kuwa: “Kupambana na vitisho katika eneo hili (la Asia Magahribi) kunahiji umoja, mshikamano na uadilifu na kujiepusha na uchochezi wa kidini.”

Kabla ya hapo, Sabah Al-Numan, msemaji wa Amirijeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Iraq, alikuwa amesema katika taarifa yake kwamba: “Kwa kuzingatia matukio yanayotokea kwa kasi kubwa katika ukanda huu na mvutano na vitisho vinavyotokana na matukio hayo dhidi ya usalama na utulivu wa eneo hili, Jamhuri ya Iraq inasisitizia msimamo wake thabiti wa kukataa kutumiwa ardhi yake, anga yake na maji yake kufanya shambulizi dhidi ya nchi yoyote ile.”

Aliongeza kuwa: “Sera ya serikali ya Iraq ni kuheshimu uhuru wa nchi nyingine na kutoingilia mambo ya ndani ya nchi hizo. Iraq imejitolea kikamilifu kuhakikisha kwamba ardhi yake haitumiki kama jukwaa la kutishia usalama na utulivu wa nchi yoyote jirani.”

Wananchi Waislamu wa Iraq nao wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba, wanapinga kutumiwa nchi yao kushambulia nchi yoyote, hasa Iran, na wanaunga mkono juhudi za kutatua kidiplomasia na kisiasa migogoro inayojitokeza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *