
Katibu Mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ametoa indhari kali kwa Saudi Arabia na Misri kuhusiana na hatua zinazochukuliwa na utawala wa kizayuni wa Israel na akasema: kinachojiri hivi sasa si suala dogo na la pembeni bali ni “tishio la kimkakati” kwa usalama wa nchi za Kiarabu na eneo kwa ujumla.
Amr Moussa ameyasema hayo alipohutubia kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Amani ya Boutros-Ghali mjini Cairo, Misri na kubainisha kwamba, kulikaribia Israel lango bahari la Bab al-Mandab ni tukio hatari sana kwa usalama wa Bahari Nyekundu.
Moussa, aliyewahi pia kuwa waziri wa mambo ya nje wa Misri amekumbusha kuwa, huko nyuma wakati wa vita vya Oktoba 1973 dhidi ya utawala wa kizayuni wa Israel, Misri ilichukua uamuzi wa kimkakati wa kuifunga njia hiyo muhimu sana ya baharini, uamuzi ambao ulikuwa na taathira ya kipekee kwa mlingano wa nguvu na usalama wa eneo.
Huku akitanabahisha kwamba utoaji taarifa tu sasa hautoshi tena, Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Arab League amesema, hali iliyopo hivi sasa ni “kengele ya hatari” kwa nchi zote mbili za Misri na Saudia na hasa kutokana na machafuko yanayoshuhudiwa kuanzia Sudan hadi Ethiopia na kusambaa hadi Pembe ya Afrika; hali ambayo ameielezea kuwa ni “mkondo wa kutia wasiwasi” ambao hauendani na maslahi ya Waarabu wala udharura wa kuwepo utulivu na uthabiti wa kikanda.
Amr Moussa amemalizia hotuba yake hiyo kwa kutoa wito kwa Ulimwengu wa Kiarabu kuchukua hatua makini itakayozingatia mustakabali wa mkakati mpana na uratibu wa dhati baina ya nchi za Kiarabu.
Aidha, amesisitiza kwamba, katika hali ya hivi sasa hakuna fursa ya kuwa na shaka na hatihati au kuwa na mitazamo ya kimigawanyiko, bali unahitajika msimamo wa pamoja na athirifu katika vitendo…/