
Katika Tanzania ya leo, mahali hatari zaidi pa kusema kwa uhuru si tena kituo cha polisi wala ukumbi wa mahakama.
Ni simu yako ya mkononi. Kila siku watu hubishana kwenye mitandao ya kijamii kama WhatsApp, hukiri kupitia ujumbe wa sauti, hutuma vitisho wakiwa na hasira na hueleza masuala nyeti kwa urahisi kupitia maandishi. Wengi huamini kuwa ujumbe unapofutwa hupotea kabisa. Kisheria, hali haiko hivyo.
Mawasiliano ya kidijitali yamekuwa kimya kimya, mojawapo ya aina zenye nguvu zaidi za ushahidi katika mahakama za Tanzania.
Picha za skrini, ujumbe wa WhatsApp, barua pepe na rekodi za sauti sasa hutumika kuthibitisha udanganyifu, vitisho, makosa ya kingono, uvunjaji wa mkataba, rushwa na hata mauaji.
Hili si jambo jipya, linasimamiwa kikamilifu na sheria. Kifungu cha 3 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Sura ya 306, kinatambua kisheria mawasiliano ya kielektroniki, wakati kifungu cha 18 cha Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, Sura ya 442, kinaeleza kuwa kumbukumbu za kielektroniki zinakubalika kama ushahidi na haziwezi kukataliwa kwa sababu tu zipo katika mfumo wa kielektroniki.
Kwa maneno rahisi, ujumbe wa WhatsApp unaweza kuwa na uzito wa kisheria sawa na barua iliyosainiwa.
Kilicho muhimu kwa mahakama si kama ushahidi umetoka kwenye simu, bali kama unaweza kuaminika.
Hapa ndipo uthibitishaji na mlolongo wa umiliki wa ushahidi vinapohusika. Mahakama lazima iridhike kuwa ujumbe au sauti ni halisi na haujabadilishwa.
Kwa kawaida, simu huchunguzwa na mtaalamu wa uchunguzi wa kidijitali ambaye huchota taarifa na kuandaa ripoti inayoonyesha namba ya simu, taarifa za akaunti, alama za muda na maudhui kamili ya mawasiliano.
Ripoti hii huunda kiungo kati ya simu na mahakama. Kifungu cha 40 (a) cha Sheria ya Ushahidi, Sura ya 6, kinaruhusu ushahidi wa kielektroniki kupokelewa ikiwa unaambatana na cheti kinachoeleza jinsi ulivyotengenezwa na kuthibitisha kuwa haujachezewa.
Hili likifanyika, picha za skrini na ujumbe wa sauti huwa na nguvu sawa na hati yoyote ya mashitaka.
Watu mara nyingi hudhani kuwa kufuta ujumbe kunawalinda. Kwa uhalisia, taarifa bado zinaweza kurejeshwa kutoka kwenye vifaa na kwa watoa huduma.
Chini ya kifungu cha 31 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao, Sura ya 443, mahakama inaweza kuamuru kampuni za mawasiliano kutoa rekodi za simu, ujumbe au taarifa za akaunti zinazohusishwa na namba ya simu au mtumiaji fulani. Mawasiliano ya kidijitali huacha alama ambazo ni vigumu sana kufuta.
Alama hizi zinaweza hata kuwaweka watu wasio na hatia katika hatari kubwa ya kisheria. Kumekuwapo matukio ambayo mtu humwomba mwingine ampigie simu mtu wa tatu na baadaye mtu huyo hukutwa amekufa.
Polisi wanapofanya uchunguzi, rekodi za simu huonyesha mtu wa mwisho kuzungumza na marehemu ni yule aliyepiga simu.
Hata kama mpigaji simu alikuwa anasaidia tu na hakuwa na uhusiano wowote na kosa, huwa mtuhumiwa kwa sababu kumbukumbu ya kidijitali inamweka katikati ya mawasiliano ya mwisho.
Hivyo, suluhisho la hili si kuacha kuwasiliana na watu, bali kuwasiliana kwa busara. Watu wanapaswa kuepuka kujadili masuala nyeti kwenye majukwaa yasiyo rasmi, waache kujieleza kwa ujumbe mrefu kwa simu, waepuke kutuma ujumbe wa sauti unaoweza kurudiwa nje ya muktadha na watafute ushauri wa kisheria kabla ya kuweka jambo lolote zito kwa maandishi.
Pale panapokuwa na shaka, ni salama zaidi kuzungumza na wakili kuliko kuandika ujumbe ambao baadaye unaweza kusomwa mahakamani.
Hatari halisi si teknolojia yenyewe, bali ni namna watu wanavyoitumia kwa uzembe. Watanzania wengi hujitengenezea ushahidi dhidi yao wenyewe bila kutambua.
Wanathibitisha mambo kwa maandishi, wanabishana kupitia ujumbe na wanaacha alama za kidijitali ambazo baadaye huwa mitego ya kisheria.
Kisheria, hili huitwa kujishtaki mwenyewe, kutoa taarifa zinazokufunga. Kanuni salama zaidi ni rahisi.
Kama usingelisema mbele ya jaji, usiiandike. Kama usingeisaini kwenye karatasi, usiitume kwenye ujumbe.
Ukimya si udhaifu. Ni kinga ya kisheria. Mahakama zetu haziongozwi tena na mashahidi waliopo kizimbani pekee.
Sasa zinasikiliza simu, zinasoma mazungumzo na kurudia ujumbe wa sauti. Mazungumzo yako yanaweza kuwa mahakama yako, na hayasahau kamwe.