Marekani. Kati ya mambo yanayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wengi duniani kote, ni kumwona Cristiano Ronaldo (40), katika Fast & Furious kama alivyodokeza mwigizaji wa filamu hizo, Vin Diesel(58), hivi karibuni.
Tangu Diesel aliposema kuna nafasi ya Ronaldo katika mfululizo wa filamu hizo, kumeibuka picha nyingi mtandaoni zilizotengenezwa na akili unde (AI) ambazo zinajaribu kutoa taswira itakavyokuwa.
Ni wazi endapo CR7 atacheza Fast & Furious, basi hilo litakuwa picha lingine la kutisha kutokana na nguvu ya ushawishi aliyonayo, bidii ya kazi na kiu ya kufikia rekodi kubwa za juu katika mafanikio.
Kinachotoa uhakika atashirikiana na Fast & Furious, ni kuwa mshambuliaji huyo wa Ureno anayepiga Al-Nassr ya Saudi Pro League, yupo mbioni kustaafu soka na tayari alishaanza kuwekeza katika filamu.
Fast & Furious au The Fast and the Furious, ni mfululizo filamu maarufu za Marekani (Hollywood) unaohusu matukio ya kusisimua kama mbio za magari za mitaani, uhalifu, wizi mkubwa na upelelezi au ujasusi.
Umaarufu wake unatokana na mbio za magari yenye kasi kubwa, magari ya kifahari na yenye nguvu, matukio hatari na ya kushangaza, na mchanganyiko wa uhalifu, ujasusi na vita dhidi ya magenge hatari.
Mradi huu ulianza mwaka 2001 chini ya kampuni ya Universal Pictures, na filamu yake ya kwanza ilitokana na makala ya Jarida la Vibe mwaka 1998, iliyoitwa ‘Racer X’ ambayo iliandikwa na Ken Li.
Racer X ni jina la mhusika wa kufikirika (fictional) lililotumika kwenye makala hiyo iliyosimulia kuhusu mbio haramu za magari mitaani (street racing) na hata maisha ya madereva wa usiku huko Marekani.
Hivyo ndivyo ilivyoanza Fast & Furious, mradi wa mfululizo wa filamu ambao kwa sasa unashikilia nafasi ya nane duniani kwa kuingiza fedha nyingi ambazo ni Dola7 bilioni, wastani wa Sh17.1 trilioni.
Hadi sasa filamu zilizoachiwa katika mfululizo huo ni 10, kuna The Fast and the Furious (2001), 2 Fast 2 Furious (2003), The Fast and the Furious: Tokyo Drift (2006) na Fast & Furious (2009).
Nyingine ni Fast Five (2011), Fast & Furious 6 (2013), Furious 7 (2015), The Fate of the Furious (Fast 8) (2017), F9: The Fast Saga (2021) na Fast X (2023).
Filamu nne za mwanzo zilijikita kwenye mbio haramu za magari mitaani na baadaye mfululizo wa filamu hizo ulibadilika (kuanzia Fast Five) na kujikita zaidi kwenye wizi wa kimataifa na ujasusi.
Miongoni mwa wahusika wake wakuu wanaofahamika na wengi ni Vin Diesel (Dominic Toretto), Paul Walker (Brian O’Conner), Dwayne Johnson (Luke Hobbs), Michelle Rodriguez (Letty), Ludacris (Tej Parker) n.k.
Ikumbukwe rapa Wiz Khalifa alitoa ngoma yake, See You Again (2015) ambayo video yake imetazamwa mara bilioni 6.8 YouTube, kwa ajili ya kumuenzi Paul Walker aliyefariki dunia kwa ajali ya gari mwaka 2013.
Hivyo hakuna shaka kuwa kuingia kwa Ronaldo kwenye ulimwengu huu mkubwa wa Fast & Furious kutakuwa ni hatua nyingine muhimu katika kuikuza zaidi chapa yake kimataifa.
“Kila mtu aliuliza iwapo [Ronaldo] atakuwepo katika ulimwengu wa Fast… Nawaambia, yeye ni mtu maana kabisa. Tulitenga nafasi kwa ajili yake,” alieleza Diesel katika ukurasa wake wa Instagram.
Kauli yake imepokelewa kwa uzito kwa sababu kuna taarifa zinazodai filamu itakayofuatia- Fast & Furious 11, inayoaminika itaitwa Fast Forever, ndio itakuwa ya mwisho katika mradi huo ulioanza 2001.
Inatajwa huwenda toleo lijalo likaingia sokoni mwakani, hivyo mambo ni mengi kwa Ronaldo kwa sababu wakati huo atashiriki Kombe la Dunia 2026, michuano itakayofanyika Marekani, Mexico na Canada.
Ronaldo kuingia kwenye tasnia ya uigizaji ni sehemu ya mustakabali wake pindi atakapostaafu na tayari alitangaza kuanzisha studio yake ya filamu, UR Marv hapo Aprili kwa kushirikiana na Matthew Vaughn.
“Ronaldo anapenda filamu, na Vaughn anapenda michezo. Wote wamekuwa mabingwa waliovunja rekodi katika fani zao, na wote wanapenda hadithi nzuri,” ukurasa wa X, zamani Twitter wake Ronaldo ulieleza.
“Wataunganisha ulimwengu wa michezo na usimuliaji wa hadithi kupitia UR Marv, studio huru ya filamu inayokumbatia teknolojia bunifu huku ikiheshimu mila na jadi,” ilieleza taarifa.
Naye Vaughn, mtayarishaji na muongozaji filamu kutokea Uingereza akijulikana zaidi kupitia mfululizo wa filamu za Kingsman na X-Men, alisema ana kiu ya kufanya kazi na Ronaldo huku akimtaja kama shujaa wa kweli.
Wawili hao kwa pamoja wamefadhili na kutayarisha filamu mbili za kusisimua na wako mbioni kuanza ya tatu katika mfululizo huo huo. Kwa sasa wanasubiri kwa hamu kutangaza rasmi ni lini filamu ya kwanza itatoka.