Dodoma. Dodoma Jiji FC inaikaribisha Tanzania Prisons katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma leo katika mechi ambayo kinyume na matokeo ya ushindi, sare au kupoteza kutaiweka timu yoyote kati ya hizo katika hali ngumu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Timu hizo zina idadi sawa ya pointi ambapo kila moja imekusanya saba ingawa zinatofautiana kwa idadi ya michezo ingawa zote zipo katika nafasi zisizoridhisha kwenye msimamo wa ligi huku tofauti ya mabao ya kufunga ikizitofautisha.
Wenyeji Dodoma Jiji wako katika nafasi ya 15 huku Tanzania Prisons ikiwa katika nafasi ya 14.
Maana yake timu itakayopata ushindi leo, itasogea hai katika nafasi ya 10 ambayo kwa sasa kuna timu ya TRA United.
Ikiwa Dodoma Jiji itashindwa kupata ushindi, itasalia katika nafasi iliyopo sasa lakini kama Tanzania Prisons itapoteza, itajikuta ikishuka kwa nafasi moja na kuangukia nafasi ya 16.
Kumbukumbu ya michezo iliyopita ya ligi msimu huu, inaonyesha kuwa Dodoma Jiji haijapata ushindi katika mechi sita mfululizo ambapo imetoka sare mara tatu na kupoteza tatu.
Tanzania Prisons yenyewe haijapata ushindi katika mechi tatu mfululizo zilizopita ambapo imepoteza mbili na kutoka sare moja ingawa kabla ya hapo ilipata ushindi mara mbili mfululizo.
Kocha wa Dodoma Jiji, Amani Josiah amesema kuwa wachezaji wake wamejiandaa vizuri kwa mchezo huo ingawa wana uhakika utakuwa mgumu.