Kikao hicho Baraza Kuu la Umoja la Mataifa killianza siku ya Jumatano (Septemba 10) kwa ufungaji wa kikao cha 79 na kuapishwa rasmi kwa rais mpya wa Baraza hilo, Annalena Bearbock, aliyechukuwa wadhifa huo wa mzunguko kutoka kwa Philemon Yang.
Yang, waziri mkuu wa zamani wa Kameruni na ambaye alishikilia nafasi hiyo kwa jina la uwakilishi wa Afrika, aliiambia hadhara hiyo kuwa mkataba ulioianzisha taasisi hiyo na Umoja wa Mataifa wenyewe ni alama ya ahadi ya pamoja kwamba “dunia inaweza kuwa bora zaidi, ikiwa viongozi watatimiza wajibu wao kuitekeleza ahadi hiyo.”
Maudhui ya kikao hiki cha 80 cha Baraza hilo Kuu la Umoja wa Mataifa, ambalo linaadhimisha pia miaka 80 tangu kuundwa kwa taasisi hiyo ni “Tukiwa wamoja, tunakuwa bora zaidi: Miaka 80 na zaidi kwa ajili ya amani, maendeleo na haki za binaadamu.”
Baerbock achukuwa uongozi
Akipokea kijiti cha uongozi wa Baraza hilo, Baerbock , aliuita mwaka huu kuwa wa “utekelezaji, mageuzi na ujenzi wa Umoja wa Mataifa unaohitajika kwa miaka mingine 80 ijayo.”
Waziri huyo wa zamani wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, ambaye anachukuliwa kuwa mwakilishi wa Ulaya, atashikilia kiti hicho kwa mwaka mmoja ujao.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres , alikumbushia kuwa dhamira ya kuundwa kwa Umoja huo haikuwa tu kuzuia vita, bali pia kupata suluhisho kwa matatizo mengine yanayoukumbua ulimwengu kama vile umasikini, njaa, maradhi na ukosefu wa usawa.
Wiki hasa itakayokuwa na hotuba za viongozi wa juu wa mataifa wanachama inatarajiwa kuanza tarehe 22 na kuendelea hadi tarehe 30 Septemba, ambapo viongozi hao watahudhuria kile kiitwacho “Mdahalo Mkuu” na matukio mengine mbalimbali.
Miongoni mwa matukio hayo ni Maadhimisho ya Miaka 80 ya Umoja wa Mataifa, Mkutano wa Maendeleo Endelevu, Maadhimisho ya Miaka 30 ya Kongamano la Nne la Wanawake Duniani, Mkutano wa Kilele wa Mabadiliko ya Tabianchi na Uzinduzi wa Mdahalo wa Ulimwengu kuhusu Usimamizi wa Akili Mnemba.