
Rais Hussein Ali Mwinyi yuko kwenye mchakato wa kuwaomba Wazanzibari wampe muhula mwingine kuwaongoza.
Dkt. Mwinyi ni mtoto wa aliyekuwa rais wa awamu ya tatu Zanzibar na awamu ya pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Ali Hassan Mwinyi.
Dkt. Hussein Mwinyi alizaliwa Disemba 23, mwaka 1966. Masomo yake ya msingi na sekondari alisoma nchini Tanzania na katika taifa la Misri.
Kitaaluma yeye ni daktari wa binaadamu ambapo alipata elimu hiyo katika Chuo Kikuu cha Marmara nchini Uturuki na baadaye kwenda nchini Uingereza alipopata shahada ya uzamili.
Amewahi kufanya kazi ya udaktari katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Aliingia kwenye siasa mwaka 1999 na baadaye akateuliwa kuwa naibu waziri wa afya katika serikali ya awamu ya tatu.
Mwaka 2005 alihamisha ngome yake ya kisiasa kutoka bara hadi visiwani na akapata ushindi kwenye uchaguzi wa mwaka huo.