Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan Kusini imesema inashirikiana na mamlaka ya Ethiopia kuwarudisha nyumbani raia 27 wanaozuiliwa katika Gereza la Muzan huko Addis Abeba.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari wa Wizara hiyo, Msemaji Apuk Ayuel Mayen alisema wafungwa hao ni wachunga ng’ombe kutoka Jimbo la Equatoria Mashariki ambao walivuka mpaka wa kimataifa bila kukusudia.
“Wizara inaratibu kurudishwa salama kwa vijana 27 kutoka Jimbo la Equatoria Mashariki ambao kwa sasa wanazuiliwa katika gereza la Muzan nchini Ethiopia,” Apuk alisema.
“Walikuwa wachungaji ng’ombe, hivyo walikuwa na silaha. Na hivyo, kupitia ubalozi wetu mjini Addis Ababa, tunafanya mazungumzo na serikali ya Ethiopia ili waachiliwe,” aliongeza.