
Watu hao akiwemo mwanaharakati mashuhuri wa Sweden Greta Thunberg wamesafirishwa kuelekea katika mataifa ya Ugiriki na Slovakia. Hata hivyo, wanaharakati hao wamelalamika kuwa walitendewa vibaya na hata kudhalilishwa walipokuwa mikononi mwa maafisa wa Israel. Rafael Borrego ni mwanaharakati kutoka Uhispania aliyekuwa kwenye msafara huo wa Flotilla :
” Tulipokamatwa, tulipitia mchakato wa kutuaibisha ambapo walichukua vitu vyetu vyote na kutuacha wengi wetu tukiwa na nguo kadhaa. Kila kitu kilifanyika kwa njia ya kutufedhehesha kwa sababu walikuwa wakitucheka na hawakutuchukulia kama binaadamu, yaani tulichukuliwa kwa uduni kuliko hata wanyama.”
Israel hata hivyo imekanusha tuhuma hizo. Hayo yakiarifiwa, mazungumzo kati ya wapatanishi wa Israel na Hamas juu ya namna ya kuumaliza mzozo wa Gaza chini ya mpango wa rais wa Marekani Donald Trump yanaendelea katika mji wa Sharm el-Sheikh nchini Misri.