
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva, nchini Uswisi, Mwakilishi wa UNHCR nchini Msumbiji Xavier Creach, amesema kuwa ongezeko hili jipya la vurugu linaashiria hatua mpya katika mzozo wa kaskazini mwa nchi hiyo.
Baada ya miaka mingi ya kutokuwa na uhakika, familia zimefika mwisho wa uvumilivu wao; baadhi wakibaki licha ya hatari, huku wengine wakilazimika kukimbia tena bila matumaini ya kurejea. Idadi ya watu zaidi ya 100,000 wamelazimika kukimbia mwaka huu pekee, na wimbi hili la hivi karibuni likiwa moja ya makubwa zaidi kuwahi kurekodiwa.
Mzozo wa muda mrefu wa Cabo Delgado
Tangu mzozo huo uanze mwaka 2017, zaidi ya watu milioni 1.3 wamelazimika kuyahama makazi yao. Kwa mara ya kwanza, wilaya zote 17 za jimbo la Cabo Delgado—eneo ambalo limekuwa kitovu cha machafuko—zimeathiriwa vibaya moja kwa moja na mashambulizi.
Mashambulizi hayo yanayofanyika kwa wakati mmoja katika maeneo mbalimbali, yamesababisha hofu na hali ya kutokuwa na utulivu. Wengi wa waliokimbia hivi karibuni walikuwa ni wenyeji waliokuwa wakihifadhi wengine, lakini sasa nao wamejikuta wakihitaji msaada wa kibinadamu.
Kuongezeka kwa hatari na vurugu dhidi ya raia
Hofu juu ya usalama inazidi kuongezeka huku raia wakiendelea kulengwa, kukiwa na ripoti za mauaji, utekaji nyara, na unyanyasaji wa kingono. Watoto ni miongoni mwa waathiriwa wakuu, huku kukiwa na taarifa za kuandikishwa kwa nguvu jeshini na mashambulizi ya makusudi kutoka kwa makundi yenye silaha yasiyo ya kiserikali.
Mwakilishi huyo wa UNCHR nchini Msumbiji amesema wanawake na wasichana wako katika hatari kubwa ya kukumbwa na unyanyasaji wa kijinsia, hasa wanapokwenda kutafuta maji au kuni mbali na maeneo ya hifadhi. Watu wenye ulemavu na wazee wamepata ugumu kukimbia wakati wa mashambulizi, na baadhi yao wameachwa nyuma.
Aidha, wengi ambao wamekimbia wanakabiliwa na dalili za msongo wa mawazo na wanahitaji msaada wa kisaikolojia haraka.
Kuongezeka kwa matukio ya usalama mwaka 2025
“Kwa mwaka huu wa 2025, ghasia zimeongezeka kwa kasi kubwa. Kufikia mwishoni mwa mwezi Agosti, idadi ya matukio zaidi ya 500 ya kiusalama yaliyowaathiri raia yalikuwa yamerekodiwa, ikiwemo uvamizi wa vijiji, utekaji nyara, mauaji, uporaji, na uharibifu wa nyumba na miundombinu,” amesema Bwana Creach, akiongeza kuwa, “idadi hii ni kubwa zaidi ikilinganishwa na matukio 435 yaliyoripotiwa mnamo mwaka 2022, ambao ulionekana kuwa moja ya vipindi vigumu zaidi vya mzozo huo.”
Mgogoro wa kibinadamu na changamoto za mabadiliko ya tabianchi
Kwa mujibu wa UNHCR, mgogoro wa kaskazini mwa Msumbiji umegeuka kuwa miongoni mwa hali ngumu zaidi za kibinadamu katika ukanda huo. Mbali na ghasia, familia zinakabiliwa na madhara ya vimbunga, mafuriko, na ukame wa muda mrefu.
Vyanzo vya mapato vimeharibiwa, bei za chakula zimepanda, na huduma za msingi zimekuwa haba. Mchanganyiko wa migogoro na athari za mabadiliko ya tabianchi umeunda mzunguko wa mateso na ukosefu wa matumaini ambao unazidi kuwa mgumu kuvunjika.
Wito kwa jumuiya ya kimataifa
Licha ya changamoto ya ufadhili duniani, Mwakilishi huyo wa UNHCR amesema kwa ushirikiano na wadau wameendelea kusaidia wakimbizi wa ndani na jamii zinazowahifadhi kaskazini mwa Msumbiji. Ofisi maalum za msaada zimeanzishwa ili kutambua watu wenye mahitaji maalum, kutoa ushauri nasaha na huduma za afya ya akili, kusambaza vifaa vya kiutu, pamoja na kusaidia familia kurejesha nyaraka zao za kiraia kwa ushirikiano na mamlaka za eneo. “Hata hivyo, hadi sasa UNHCR imepokea kiasi cha dola milioni 66 pekee kati ya dola milioni 352 zinazohitajika mwaka huu, hali inayoodhoofisha uwezo wa kutoa huduma wakati mahitaji yakiongezeka.” amesema.
Kwa mujibu wa UNHCR, miaka minane tangu machafuko kuanza, ongezeko hili jipya la vurugu ni kumbusho tosha kwamba mgogoro wa kaskazini mwa Msumbiji bado haujamalizika. Maelfu ya familia zimeendelea kuhama mara kwa mara, zikijaribu kujenga upya maisha, lakini zikijikuta zikiyakimbia tena. UNHCR imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada wake kwa Msumbiji, ikisisitiza umuhimu wa kulinda raia, kurejesha upatikanaji wa huduma muhimu, na kuwekeza katika suluhisho za kudumu ili kuzuia mateso zaidi.