Mkutano huo ulipangwa kufanyika Ikulu ya Antananarivo muda mfupi baada ya Rais Rajoelina kumteua Jenerali wa jeshi Ruphin Fortunat Dimbisoa Zafisambo kuwa waziri mkuu mpya katika juhudi za kupunguza maandamano ya kupinga serikali ambayo tayari yamesababisha vifo vya watu 22, kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo uteuzi huo haukupokelewa vyema na wengi na mamia ya waandamanaji walijitokeza tena mitaani wakilalamikia kwamba hatua hiyo ni dalili ya serikali kutaka kudhibiti nchi kwa mkono wa kijeshi
Kundi linaloongoza maandamano ya GenZ lasema halitashiriki
Kundi la vijana lijulikanalo kama Gen Z Mada, ambalo linaongoza maandamano hayo lilisema kwenye mitandao ya kijamii kuwa linakataa kile lilichokiita “mazungumzo ya hadaa” kutoka kwa “serikali inayowakandamiza na kuwanyanyasa vijana mitaani.” Limesema halitoshiriki katika mazungumzo yoyote hadi sauti za wananchi zitakaposikilizwa.
Maandamano ya GenZ yalianza Septemba 25 kufuatia hasira za wananchi kutokana na kukatika mara kwa mara kwa umeme na maji, lakini yameongezeka na kugeuka kuwa vuguvugu la upinzani wa kisiasa linalomkosoa rais kwa kushindwa kutatua matatizo ya msingi ya wananchi.
Waandamanaji wagomea hatua zilizochukuliwa
Licha ya Rajoelina kuivunja serikali yake wiki iliyopita na kisha kuwateua mawaziri watatu wapya wanaosimamia ulinzi na usalama wa ndani, waandamanaji wamesema hatua hizo hazijajibu mahitaji yao halisi. Wameitaka serikali kuomba radhi hadharani kwa ukatili uliofanywa dhidi ya waandamanaji na kurekebisha mfumo wa mahakama ya katiba pamoja na kuvunja baraza la seneti.
”Waziri Mkuu mpya? Sio tunayemtaka, tunataka mabadiliko ya mfumo Je, huyo Waziri Mkuu atashuka huku chini aje kuwahudumia wananchi wa Madagascar? Hapana! Anaweza kufanya nini? Atabadilisha nini? Atabadilisha nini ndani ya miezi sita? Nimeona Rais amempa miezi sita kupima uwezo wake; ataweza kufanya nini muda huo? Atatupandishia mishahara? Basi, tutasubiri tuone; kama hataondolewa kwanza” amesema mwanafunzi wa udaktari mwenye umri wa miaka 25 ambaye hakutaka kutambulishwa.
Wakati huo huo Rais Andriy Rajoelina amesema nchi yake “haitaki tena vurugu bali inataka amani,” huku akiwataka vijana kuhudhuria mkutano wa hadhara Ikuluni “ili kuuliza maswali na kueleza maoni yao kwa uhuru.” Hata hivyo, kundi la Gen Z Mada limesema litaisubiri serikali hadi Jumatano usiku itoe majibu ya kuridhisha, la sivyo litaitisha mgomo wa kitaifa.
Wachambuzi wanasema hatua ya rais kumteua afisa wa jeshi inaashiria jaribio la kuimarisha umoja ndani ya vyombo vya ulinzi, lakini pia inaweza kuchochea hofu ya kurejea kwa utawala wa kijeshi. Wengine wameonya kwamba endapo serikali haitasikiliza madai ya vijana, maandamano yanaweza kuendelea kwa miezi kadhaa.