MSHAMBULIAJI wa Mbeya City, Habib Kyombo amesema kuwa yajayo ndani ya timu hiyo yanafurahisha, huku akiwatoa hofu mashabiki kutokana na majeraha aliyoyapata.

Kyombo ambaye ametua Mbeya City msimu huu akiwa amesaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine, rekodi zake zinaonyesha aliwahi kuzichezea timu za Pamba Jiji, Simba, Fountain Gate na Singida Black Stars.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kyombo alisema maisha ndani ya Mbeya City yako tofauti ikilinganishwa na alikotoka kwani kila sehemu ina mazingira, wachezaji, makocha na vitu vingine vyenye tofauti na alikokuwa.

Alisema kuwa aliumia kukosa mechi muhimu dhidi ya Yanga kwa sababu ya majeraha ya nyonga, lakini anamshukuru Mungu kwamba licha ya kuikosa wapinzani wao hawakuweza kuwadhuru.

“Nilipata majeraha baada ya kuumia nyonga, ila baada ya siku tano daktari amesema nitarejea katika hali yangu ya kawaida. Hata hivyo, bado timu inaendelea na mazoezi,” alisema Kyombo.

“Ninachofurahia zaidi Mbeya City ni kupata nafasi ya kucheza jambo ambalo ni zuri kwa mchezaji yeyote kuona anafanyia kazi kile kilichompeleka kwenye timu husika.”

Aliongeza kuwa, “naamini sana kwenye mwendelezo mzuri ambao timu yetu unao. Natumaini kabisa tutafanya vyema kwani tumepoteza mchezo mmoja kati ya mitatu, sio rekodi mbaya.”

Mbeya City ambayo imepanda Ligi Kuu Bara msimu huu imecheza mechi tatu hadi sasa ikiwa na rekodi ya kutoka suluhu katika michezo miwili dhidi ya Singida Black Stars na JKT Tanzania, na kufungwa mabao 2-0 na Azam FC.

Kikosi hicho kinashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi kikiwa na pointi nne katika michezo mitatu kiliyocheza, huku kinara ikiwa Simba yenye alama sita katika mechi mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *