Miaka ya nyuma, magonjwa kama kisukari na shinikizo la damu yalikuwa yakihusishwa zaidi na watu wazima wenye umri wa miaka 40 na kuendelea.

Yalichukuliwa kama maradhi ya uzee, matokeo ya mwili kuchoka kutokana na maisha marefu. Lakini hali imebadilika kwa kasi ya kutisha.

Sasa, yale magonjwa yaliyokuwa yakionekana mbali yamekuwa wageni wa karibu katika maisha ya vijana. Kifo kimeanza kuwa karibu na kizazi ambacho kilipaswa kuishi kwa nguvu na kutimiza ndoto zao. Vijana wananyemelewa na maradhi haya, na kibaya zaidi, wengi hawajitambui kwa kuwa wametingwa na na starehe, ulevi, uvivu na mitindo mibaya ya maisha.

Kisukari na shinikizo la damu ni magonjwa yanayojulikana kimataifa kama “wauaji wa kimya.” Hayaingii kwa kelele; huingia taratibu bila ishara kubwa za mtu kushtuka.

Kwa kawaida, mtu huanza kujisikia dalili pale ambapo ugonjwa umeshaota mizizi na kuharibu viungo vya mwili.

Zamani, vijana walijulikana kwa afya njema, misuli imara, na nguvu za kutekeleza shughuli nyingi. Lakini sasa, kutokana na mabadiliko ya kimaisha, idadi ya vijana wanaogundulika na kisukari au shinikizo la damu imeongezeka kwa kasi isiyo ya kawaida.

Wataalamu wa afya wanasema sababu kubwa ni mabadiliko ya mtindo wa maisha. Vijana wengi wa sasa hawana tena hamasa ya kufanya mazoezi, chakula chao kimejaa mafuta na sukari, na muda mwingi hutumika kwenye simu, runinga, michezo ya kompyuta badala ya kukimbia viwanjani.

Matokeo yake, uzito kupita kiasi, lehemu nyingi mwilini na udhaifu wa kinga, vimekuwa kawaida kwa vijana.

Mtego wa mtindo wa maisha

Ulevi, uvutaji wa sigara, na matumizi ya dawa za kulevya vimekuwa sehemu ya maisha ya baadhi ya vijana. Wengine huamini kuwa bila kunywa pombe au kuvuta bangi, hawawezi kuonekana “wa kisasa” au “wa mjini.”

Matumizi ya vilevi yanaharibu ini, moyo na figo, huku yakichochea zaidi uwezekano wa kupata shinikizo la damu na kisukari.

Starehe zisizo na kikomo pia ni adui wa afya. Vijana wengi hutumia muda mwingi kwenye klabu za usiku, kula vyakula vya haraka na kunywa soda kwa wingi. Vyakula hivi havina lishe muhimu bali vinaongeza sukari na mafuta mwilini. Hali hii inasababisha kupanda kwa uzito kupita kiasi, jambo linaloongeza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza.

Pia, kizazi cha sasa kimezama katika ulimwengu wa teknolojia. Ni rahisi kuona kijana akiketi kwa saa nyingi akitazama video, akicheza michezo ya mtandaoni, au kupiga soga kwenye mitandao ya kijamii.

Mwili wake hauna harakati za kutosha, mishipa ya damu inalegea, na mapafu hayapati nafasi ya kupumua kwa kina. Kimsingi, mwili unakufa kimya kimya.

Kibaya zaidi ni kwamba vijana wengi hawajitambui. Wanaishi kana kwamba afya yao ni mali isiyoharibika. Hawajali uchunguzi wa kiafya wa mara kwa mara, hawashughulikii dalili ndogo kama kichwa kuuma au uchovu wa mara kwa mara. Kila kitu huchukuliwa kama kawaida ya maisha ya kila siku. Wengi husema, “Hii ni homa ndogo tu” au “labda nimechoka.” Ndipo ugonjwa unapotambuliwa wakiwa tayari wameshaingia hatua hatarishi.

Kutojitambua huku kunasababisha vijana wengi kupoteza maisha mapema. Wengine hupooza ghafla kutokana na kiharusi  kinachosababishwa na shinikizo la damu lisilodhibitiwa. Wengine hupoteza kuona kwa sababu ya kisukari, na wengine hupoteza nguvu za viungo kutokana na matatizo ya mishipa ya damu.

Matokeo kwa jamii

Kifo cha kijana siyo hasara kwa familia pekee bali kwa taifa zima. Vijana ndio nguvu kazi ya taifa, ndio mabega ya kubeba uchumi na maendeleo. Taifa lenye vijana wagonjwa ni taifa dhaifu. Maisha yanapokoma mapema kutokana na magonjwa yanayozuilika, ndoto za familia, mipango ya maendeleo, na nguvu kazi hupotea. Ni sawa na kuzima taa wakati giza linapoanza kutanda.

Vijana wafanye haya

Hali hii inaweza kubadilishwa ikiwa vijana wataamua kubadilisha mienendo yao ya maisha. Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia:

Mosi, mazoezi ya mwili: Mazoezi ni tiba na kinga. Kila kijana anapaswa kuhakikisha anafanya mazoezi angalau dakika 30 kila siku iwe ni kutembea kwa kasi, kukimbia, kuogelea, kucheza mpira, au kufanya mazoezi ya viungo. Mazoezi husaidia kudhibiti uzito, kupunguza sukari na shinikizo la damu, na kuimarisha moyo.

Pili, lishe bora: Vijana wanapaswa kujiepusha na vyakula vyenye mafuta mengi, sukari nyingi na chumvi kupita kiasi. Mboga za majani, matunda, nafaka zisizokobolewa na protini safi kama samaki, kuku au kunde vinapaswa kuwa sehemu ya mlo wa kila siku. Kunywa maji mengi badala ya soda na juisi za viwandani.

Tatu, kuepuka vilevi na dawa za kulevya:

Hakuna faida ya kudumu katika ulevi na dawa za kulevya. Badala ya kupoteza afya na heshima, kijana anaweza kuwekeza nguvu na muda huo kujijenga kielimu na kiuchumi.

Nne, kupunguza msongo wa mawazo:

Vijana wa leo hukumbwa na changamoto nyingi kama ukosefu wa ajira, shinikizo la maisha, na matarajio ya kijamii. Hata hivyo, msongo wa mawazo unapodhibitiwa vibaya, huchochea magonjwa kama shinikizo la damu.

Ni muhimu kujifunza mbinu za kupunguza msongo kwa kusali, kutafakari, kushirikiana na marafiki wenye ushauri mzuri, na kufanya mambo yanayoleta furaha chanya.

Tano, uchunguzi wa afya:

Kila kijana anapaswa kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara hasa kipimo cha sukari ya damu, shinikizo la damu, uzito na vipimo vingine muhimu. Uchunguzi wa mapema unaweza kusaidia kudhibiti ugonjwa kabla haujaleta madhara makubwa.

Sita, kujitambua:Hatua ya kwanza ya kuishi maisha marefu yenye afya ni kujitambua. Vijana wanapaswa kuelewa kuwa miili yao siyo chuma. Afya ni mali, na bila afya hakuna ndoto inayoweza kufanikishwa.

Nafasi ingalipo kwa vijana

Vijana wananyemelewa na kifo kisichotarajiwa kupitia magonjwa ambayo zamani yalikuwa ya wazee. Kisukari na shinikizo la damu vimekuwa wanyama wakali wanaotafuna ndoto za kizazi cha sasa.

Lakini bado kuna nafasi ya kuokoa kizazi hiki. Hatua ndogo za kubadilisha mtindo wa maisha zinaweza kuleta mabadiliko makubwa.

Kijana anapochagua kula vizuri, kufanya mazoezi, kuepuka vilevi, na kujitambua, anachagua kuishi maisha marefu yenye afya na matumaini.

Kila kijana anapaswa kujiuliza: Ninataka kufa mapema nikiwa na ndoto zisizotimia, au kuishi muda mrefu nikiwa na afya, furaha na mafanikio?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *