
Maambukizi ya njia ya mkojo yaani Urinary Track Infections kifupi UTI, si maambukizi yanayoenezwa kwa njia ya kujamiana yaani Sexual Transmitted Infection kifupi STI.
Hata hivyo, kujamiana na harakati zake huongeza hatari ya kupata UTI, hivyo kusababisha mkanganyiko na magonjwa ya STI.
UTI ni maambukizi ya bakteria kwenye mfumo wa mkojo unaohusisha kibofu, mirija inayoleta mkojo katika kibofu, figo na mrija unaotoa mkojo nje.
Eneo linaloathirika zaidi ni kibofu, wanawake wakiwa waathirika zaidi.
Hii ni kwa sababu ya kuwa mrija mfupi wa mkojo na sehemu hizo kuwa karibu na njia ya haja kubwa ambapo kuna bakteria rafiki wanaosaidia kusanisi haja kubwa ambao ndio kinara wa kusababisha UTI.
Pia UTI hutokea wakati bakteria wameshikamana katika mikono michafu au ngozi huingia kwenye mrija wa mkojo na kusafiri hadi kwenye kibofu au sehemu nyingine za mfumo wa mkojo. Ndio maana watoto hupata UTI kirahisi kwa sababu ya kujisaidia na kukosa usafi.
Wanaume si waathirika wa UTI kwa sababu ya kuwa na mrija mrefu, jambo linalowapa safari ndefu bakteria kufika katika kibofu. Mara nyingi kabla ya kusafiri husombwa na mkojo wakati wa kwenda haja ndogo.
Vile vile wanaume vijana ni nadra kupata UTI, walio katika hatari ni wenye umri mkubwa ambao wameanza kupata tezi dume na matatizo mengine ya mfumo wa mkojo.
Wakati magonjwa yanayoenea kwa kujamiana STI ni magonjwa yanayoenezwa kwa njia ya kujamiiana na huathiri mrija wa mkojo, tezi dume, mrija wa mbegu na kokwa kwa wanaume.
Wakati STI kwa wanawake ni ukeni, shingo ya kizazi, nyumba ya uzazi, mirija ya mayai na ovari.
Wanaume na wanawake wanaweza kupata STI nje juu ya ngozi kwenye sehemu za siri. Hii haitokei kwa UTI kwani hainei kwa kugusana.
Mwenza mmoja anapopata maambukizi ya UTI atatibiwa yeye tu kwa sababu hainezwi kwa kujamiana, tofauti na STI mwenza hulazimika kwenda na mwenza aliyejamiana naye kwa ajili ya kutibiwa, lengo ni kukata mnyororo wa maambukizi.
STI na UTI kuna baadhi ya dalili zinaingiliana, kama vile maumivu na hisia kuwaka wakati wa kukojoa. Hii ni moja sababu ya baadhi kuchanganya na kutojua ni UTI au STI.
UTI husababishwa na bakteria wakati Magonjwa ya STI yanaweza kusababishwa na bakteria, parasaiti na virusi, au vimelea vinavyosambazwa wakati wa kujamiiana na mwenye maambukizi.
Vile vile wakati wa kujamiana, kutokea kwa michubuko nje ya uke inaweza kuwa mazalia ya baadhi ya vimelea wa STI na hapo baadaye hupata nafasi kwenda kuleta uambukizi wa UTI kwa wanawake.
UTI kwa kawaida hutibiwa na antibiotics. STI ina matibabu mbalimbali kulingana na vimelea, ikiwamo antibiotics kwa bakteria na parasaiti, na dawa za kuzuia virusi.
Ukipata dalili zinazoashiria magonjwa ya STI na UTI, na dalili kama vile mchozo mweupe kwenye njia ya mkojo, malengelenge au vipele sehemu za siri, fika mapema katika huduma za afya.