
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kuufungulia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora ambao ulifungiwa siku 20 zilizopita kutokana na eneo lake la kuchezea kuonekana halikidhi viwango.
Kufunguliwa kwa Uwanja huo kunaufanya uwe tayari kutumika kwa mechi za nyumbani za Tabora United ikiwemo dhidi ya Simba, Oktoba 30, 2025.
Taarifa ambayo imetolewa na TFF leo imefafanua kwamba Uwanja huo umefunguliwa baada ya marekebisho yaliyofanywa kuurudisha katika hadhi nzuri.
“Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeufungulia uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora kutumika kwa michezo ya Ligi baada ya kufanya marekebisho yaliyokidhi vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.
“Uwanja huo uliofungiwa kutokana na miundombinu yake kutofaa kutumika kama ilivyoainishwa
kwenye masharti ya Kanuni ya Leseni za Klabu umekaguliwa na kukidhi vigezo vya Kikanuni
baada ya marekebisho yaliyoelekezwa kufanyika.
“TFF inaendelea kuzikumbusha klabu kuendelea kuboresha na kutunza miundombinu ya viwanjavyao vya nyumbani kwa kushirikiana na wamiliki (kwa klabu ambazo hazimiliki viwanja), ilimichezo ya Ligi ichezwe kwenye viwanja bora vinavyosaidia kuongeza shindani na thamani ya Ligi.
“Kwa taarifa hii, timu zote zilizokuwa zikitumia wanja huo kama uwanja wa nyumbani zinaweza
kuendelea kucheza michezo yake kwenye uwanjani huo,” imefafanua taarifa hiyo ya TFF.
Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ulifungiwa Septemba 20, 2025, baada ya kutumika kwa mchezo mmoja tu wa ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ambao ulikuwa baina ya TRA United na Dodoma Jiji.
Katika mechi hizo, timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2 na baada ya hapo, Tabora United ambayo ndio inatumia uwanja huo kwa mechi za nyumbani, ikawa na mechi ya ugenini dhidi ya Pamba Jiji.