
Tuzo ya kimataifa ya amani ya Nobel imetolewa kwa mwanasiasa wa upinzani na mwanaharakati wa demokrasia nchini Venezuela, Maria Corina Machado, kamati inayotoa tuzo hiyo imetangaza.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Machado amepewa heshima hiyo “kutokana na kazi zake endelevu za kupigania na kuhamasisha haki za kidemokrasia kwa raia wa Venezuela pamoja na harakati zake zinazolenga kufikia usawa na mabadiliko ya amani ya kutoa utawala wa kimabavu na kuwa wa kidemokrasia”, alisema Jorgen Watne Frydnes, mwenyekiti wa kamati hiyo iliyoko Oslo, Norway.
Kamati hiyo imesema Machado amekuwa kiungo muhimu katika kuunganisha nguvu za upinzani, ambao wakati mmoja walikuwa wamegawanyika kufuatia ukandamizwaji mkubwa waliokuwa wanapitia chini ya utawala uliopo, na sasa wanapitia hali tete ya kibinadamu na kiuchumi.
Aidha kamati hiyo imemsifu kama mmoja ya watu wakupigiwa mfano kwenye eneo la Latin Amerika, ikisema harakati zake zikimfanya alazimike kuishi nje ya nchi yake kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Tuzo hii imetolewa wakati ambapo rais wa Marekani, Donald Trump, tangu awali hakuficha tamaa yake ya kutaka kutunukiwa tuzo hiyo mwaka huu.
Tangu arejee madarakani kwa muhula wa pili mwezi Januari mwaka huu, Trump mara kadhaa amenukuliwa akisema anastahili kupewa tuzo hiyo kwa kuhusika kwake katika juhudi za kusaka suluhu ya mizozo kadhaa ya dunia ikiwemo ule wa Ukraine, Sudan, DRC na sasa vita ya Gaza.
Hata hivyo kuelekea utolewaji wa tuzo hizo Ijumaa hii, wataalamu wanaoratibu tuzo hizo, walisema hakuna uwezekano ambapo Trump anaweza kutunukiwa tuzo hiyo, wakisema será zake zinakinzana kabisa na muongozo wa namna huwa wanatoa tuzo hizo.
Mwaka uliopita tuzo hiyo ilitolewa kwa shirika moja la nchini Japan ‘Nihou Hidankyo’ linalojihusisha na harakati za kupinga matumizi ya nyuklia, shirika hili likianzishwa na wahanga wa shambulio la bomu la Hiroshima na Nagasaki.
Tuzo hii huambatana na medali ya dhahabu, cheti na zawadi ya dola za Marekani milioni 1.2.
Sherehe rasmi za kuikabidhi tuzo hiyo zinatarajiwa kufanyika Desemba 10 wakati wa maadhimisho ya kumbukizi ya mwaka 1896 ya kifo cha mwanzilishi wa tuzo hizi raia wa Uswidi, Alfred Nobel.
Alhamisi ya juma hili tuzo ya Nobel upande wa fasihi, ilitolewa na kwa mwandishi nguli Laszlo Krasznahorkai, anayetajwa na raia wengi wa Hungary kama mwandishi pakee aliye hai, na ambaye kazi zake zilijikita katika kuangazia masuala ya haki.