Dar es Salaam. Video na picha watu maarufu na wenye ushawishi zimegeuka mwalimu mpya wa urembo, hali inayosababisha wanawake wengi kuangukia kwenye uraibu wa vipodozi.

Kila uchao wakihangaika kununua bidhaa mpya za ngozi zinazotangazwa wakiamini ndizo tiketi ya kuwa na ngozi laini, ang’avu na yenye mvuto.

Kile kinachoitwa ‘skin care routine’ yaani utaratibu wa kila siku wa kutunza ngozi kimekuwa sehemu ya maisha ya wanawake wengi wanaotamani kuwa na ngozi laini, ang’avu na isiyo na makunyanzi.

Hata hivyo, nyuma ya urembo huu, kuna gharama kubwa za kifedha, muda, na hata athari za kiafya na kisaikolojia zinazojitokeza kwa baadhi ya watumiaji.

Miongoni mwa sababu zinazochochea hali hii ni kuongezeka kwa ushawishi wa mitandao ya kijamii, video na picha zinazopamba Instagram, TikTok na YouTube, zikigeuka darasa la urembo kwa wanawake wengi.

Amina Said ambaye ni mkazi wa Kinondoni anasema alianza kutumia bidhaa za kutunza ngozi baada ya kuona wasanii na watu maarufu wakionyesha ngozi zao nzuri kupitia mitandao ya kijamii hivyo na yeye akatamani kuwa kama wao.

Anasema kwa mwezi hutumia takribani Sh200,000 kununua vipodozi maarufu kama vipako, kwa ajili ya ngozi ya uso na mwili, vinavyohusisha cleanser, toner, serum, moisturizer na mafuta.

“Kuna bidhaa nyingine zinamalizika haraka, na ukiacha kutumia ngozi inabadilika, hivyo inakulazimu kuendelea,” anasema Amina.

Kwa upande wake Mariam Jumaa, mkazi wa Kinondoni, anasema amejaribu bidhaa zaidi ya 10 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kwa lengo la kupata ngozi laini na yenye mng’ao, lakini hajaona matokeo anayoyatarajia.

“Kila ninaposikia bidhaa mpya imeingia sokoni, ninajaribu. Wakati mwingine inanifanya nigharimie hadi Sh100,000 kwa wiki kununua mafuta, seramu na sabuni maalumu. Mwisho wa siku ngozi yangu inabadilika kidogo tu au inapata vipele,” anasema Mariam kwa huzuni.

Kwa upande wake, Rehema Mushi amesema aliingia kwenye mtego wa matangazo yanayodai kuwa bidhaa fulani zinatibu haraka chunusi na makovu. Alijikuta akitumia zaidi ya Sh600,000 ndani ya miezi mitatu bila mafanikio.

“Nilinunua bidhaa mtandaoni baada ya kuona video za ‘influencers’ wakizisifia. Lakini badala ya kusaidia, ziliniletea madoa. Nilijuta sana,” amesema Rehema.

Baadhi ya wanawake wameamua kuachana kabisa na matumizi ya bidhaa nyingi baada ya kuona hazileti tofauti, mfano wa hao ni Lilian Michael mkazi wa Mbezi, ambaye baada ya kuhangaika na bidhaa za vipodozi kwa muda mrefu aliamua kurudi kwenye njia za asili kama kutumia mafuta ya nazi na asali.

“Nilichoka kutumia bidhaa nyingi ambazo matokeo yake hayana uhakika. Sasa natumia asili na ninajisikia vizuri zaidi, bila wasiwasi wa kuharibu ngozi au kutumia fedha nyingi,” anasema Lilian.

Wataalamu wa masuala ya jamii wanasema changamoto kubwa dhana ya urembo wa mitandaoni, ambapo wanawake wanajilinganisha na picha zilizohaririwa kwa lengo la kuongeza mvuto, hali inayosababisha wengi kutumia bidhaa nyingi za vipodozi wakitafuta kufanana na mwonekano wa kwenye picha.

Daktari bingwa wa ngozi, Rukia Masiti anasema changamoto ya bidhaa nyingi za vipodozi ni kuwa na kemikali hatari kwa ngozi na wengi hutumia bila kujua kilichomo ndani yake na madhara yanayoweza kutokea.

“Tatizo ni kwamba wanawake wengi hununua bidhaa bila kujua viambato vilivyomo. Baadhi zina kemikali hatari kama hydroquinone na mercury, ambazo zinaweza kuharibu ngozi au hata kuathiri viungo vya ndani,” anasema.

Mtaalamu huyo amebainisha kuwa hali hiyo inasababisha wagonjwa wengi wanaofika kliniki kwake kwa ajili ya matibabu ya ngozi hubainika kuwa chanzo chake ni matumizi ya vipodozi

“Wengine wanaanza kwa ngozi kung’aa, lakini baada ya miezi michache wanaanza kupata madoa, michirizi na chunusi za kudumu haya ni matokeo ya kutumia bidhaa isiyoendana na ngozi. Bidhaa bora ni ile inayoendana na ngozi siyo inayotangazwa zaidi au maarufu mtandaoni,” amesema.

Kisaikolojia imekaaje

Wataalamu wa saikolojia wanasema wanawake wengi hujihusisha na bidhaa hizo za kutunza ngozi si tu kwa sababu ya urembo, bali pia kwa hisia ya kujiamini na utulivu wa akili.

Kufuatia hilo, wameshauri kuwa ni muhimu kwa wanawake kutambua kuwa urembo wa kweli hauishii kwenye ngozi pekee, bali unatokana pia na afya ya mwili, akili na mtazamo chanya kuhusu nafsi.

“Kuna wanawake wanaona utunzaji wa ngozi ni sehemu ya kujitunza kisaikolojia. Inawasaidia kujisikia vizuri, hasa katika mazingira yenye msongo wa mawazo,” ameeleza mwanasaikolojia Sarah Mlowe.

Hata hivyo, mtaalamu huyo anaonya kuwa shinikizo la kijamii na la kibiashara, limebadilisha dhana ya kujijali kuwa biashara inayowalazimisha wanawake kujiona hawajakamilika bila bidhaa fulani.

Kwa upande wake mwanasaikolojia Asha Mboya, anasema kwa wanawake wengi, kufanya utaratibu wa kutunza ngozi ni zaidi ya kujipodoa ni aina ya tiba ya kiakili inayowasaidia kujisikia vizuri, kupunguza msongo wa mawazo na kuongeza kujiamini.

“Wanawake wanapohisi ngozi yao ni safi na yenye mwonekano mzuri, hujengeka kisaikolojia kuwa wanavutia, jambo linaloongeza hisia chanya na kuwapa utulivu wa ndani.

“Kama utaratibu wa utunzaji ngozi unakusaidia kujipenda na kuwa na amani ya ndani, basi ni jambo zuri. Lakini ukianza kuhisi wasiwasi, hofu au aibu bila vipodozi, hapo panahitaji msaada wa kisaikolojia,” amesema Asha.

Peter Lwiza, mtaalamu mwingine wa Saikolojia Jamii ameeleza kuwa jamii imekuwa ikiwapa wanawake shinikizo kubwa kuhusu mwonekano, hali inayochangia wengi wao kuwekeza muda na fedha katika bidhaa za vipodozi.

Hata hivyo, anasema si wote wanaofanya hivyo kwa presha ya kijamii; wengine hufanya kama sehemu ya kujitunza na kujiheshimu.

“Kuna wanawake wanaotumia bidhaa hizo kama njia ya kujipongeza na kujipa nafasi ya kujijali. Hii ni muhimu kwa afya ya akili, mradi tu haigeuki utegemezi unaoathiri uchumi au kuleta hofu unaposhindwa kumudu gharama,” anaeleza Lwiza.

Biashara ya vipodozi yapamba moto

Hali hiyo imesababisha vipodozi kugeuka lulu na biashara kubwa. Katika maduka mengi ya urembo jijini Dar es Salaam na kwingineko, bidhaa za kutunza ngozi zimepanda bei kutokana na ongezeko la uagizaji kutoka nje ya nchi.

Bidhaa kutoka Korea Kusini, Marekani na Ufaransa ndizo zinazoongoza kwa mauzo, zikifuatwa na zile za China ambazo ni nafuu zaidi.

Kwa upande wa wafanyabiashara, hii ni fursa ya dhahabu huko mitandaoni maduka kadha wa kadha yanatanga zabidhaa za vipodozi kwa kutumia maneno ya kuvutia na kushawishi wafuatiliaji.

Wengine wamefungua maduka makubwa katika maeneo mbalimbali wakihusisha huduma za ushauri wa ngozi na majaribio ya bure.

Akizungumza na Mwananchi, Neema Lugano, mmiliki wa duka la urembo la Pure Skin Haven, amesema wateja wake wengi ni wanawake wanaofanya kazi ofisini.

Mfanyabiashara huyo amekiri kuwa biashara hiyo kwa sasa ina faida kubwa, hasa kutokana na bidhaa ndogo zenye thamani kubwa.

“Wanawake wengi wanajali mwonekano wao kwa sababu ya kazi. Wengine ni watumishi wa benki, mashirika ya umma na sekta binafsi. Wanataka kuonekana wasafi, warembo na wa kujiamini, hivyo kwao si tatizo kutumia kiasi chochote cha fedha kununua kipodozi kizuri.

“Mteja anachotaka umuhakikishie ni ubora wa bidhaa unayomuuzia. fedha si tatizo. Unaweza kukuta Serum ndogo ya mililita 30 inauzwa hadi Sh80,000 kwa anayejua vipodozi na kujali ngozi yake wala halalamiki,” anasema.

Zuhura Mrope, mfanyabiashara wa vipodozi katika maduka ya Kariakoo, Dar es Salaam, anasema biashara hiyo kwa sasa inalipa zaidi kuliko hapo awali.

Mfanyabiashara huyu amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, biashara ya vipodozi imeongezeka maradufu kutokana na ongezeko la matumizi ya bidhaa za kutunza na kulinda ngozi na vipodozi vya kuongeza mwonekano wa ngozi.

“Wateja wangu wengi ni wanawake wa kuanzia miaka 20 hadi 40. Wengine wanakuja na orodha waliyopata huko mitandaoni. Wengine wanataka bidhaa za kuondoa doa, wengine za kung’arisha ngozi,” anasema Zuhura.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *