Unguja. Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imekaribisha maombi ya wapigakura watakaohusika na upigaji kura ya mapema kwa kuzingatia vigezo vilivyoanishwa na Sheria ya Uchaguzi namba nne ya mwaka 2018.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, kifungu cha 82 (2), wapigakura hao ni wale wanaotekeleza majukumu yao ya uchaguzi wakiwemo wasimamizi wa uchaguzi, msimamizi msaidizi wa uchaguzi, msimamizi wa kituo, askari polisi, mjumbe au mtendaji wa Tume.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ZEC, maombi hayo yanapaswa kuwasilishwa kuanzia leo Oktoba 10, 2025 katika ofisi za uchaguzi za wilaya ambayo taarifa za mpigakura husika zinapatikana.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar, Thabit Idaous Faina, inaeleza kwamba mwombaji anatakiwa kujaza fomu ya maombi inayopatikana kwa msimamizi wa uchaguzi kwa kila wilaya au kupakua kupitia tovuti ya Tume: www.zec.go.tz.

“Mwombaji anatakiwa aainishe jimbo na kituo alichoandikishwa kupiga kura katika maombi yake na mwisho wa kuwasilisha maombi ni Oktoba 18, 2025,” amesema Faina.

Kura ya mapema Zanzibar inatambuliwa na Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2018 kifugu cha 82 (1) kwa kuchagua Rais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani.

Kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, upigaji kura wa mapema utafanyika Oktoba 28, 2025, siku moja kabla ya upigaji kura wa pamoja kwa kufuata maelekezo ya kanuni ya uchaguzi ya mwaka 2025 kuanzia kifungu cha 38 hadi 47 na kwa kufuata utaratibu uliopangwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.

Wakati huohuo, Tume ya Uchaguzi Zanzibar imesema tayari vifaa vyote vitakavyohusika na uchaguzi vimekamilika na vimewasilishwa katika ofisi zote za wilaya.

Akizugumza baada ya kufanya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi, amezitaka ofisi za wilaya kuhakikisha wanavitunza kwa umakini vifaa vya kupigia kura vilivyokabidhiwa katika ofisi zao ili vitumike kwa ufanisi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwisho wa mwezi huu.

Amesema tayari Tume imekabidhi vifaa muhimu kwa ofisi za wilaya hizo, ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Vifaa hivyo ni pamoja na masanduku ya kura na vifaa vya kuhesabia kura na vifaa vingine ambavyo vimepangwa kutumika siku ya uchaguzi.

Hata hivyo, amesema bado karatasi za kupigia kura na wino maalumu, ambavyo vipo katika hatua za mwisho za maandalizi na vitakabidhiwa muda wowote.

“Mchakato wa maandalizi ya vifaa hivi umekamilika kwa asilimia kubwa, tumebakiza tu karatasi za kura na wino, ambavyo navyo vitawasili muda mfupi ujao,” amesema Jaji Kazi

Amesema Tume imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unafanyika kwa uwazi, uhuru na amani bila changamoto zozote za kiufundi au upungufu wa vifaa.

Amesema ni muhimu watendaji wa Tume kuwa na uwajibikaji wa hali ya juu, kwani maandalizi ya vifaa ni sehemu muhimu ya mafanikio ya uchaguzi.

“Tunataka kila kitu kiwe tayari mapema, hii itasaidia kuepuka usumbufu siku ya kupiga kura na kuhakikisha wapigakura wanatekeleza haki yao kwa utulivu,” amesema.

Katika ziara hiyo, mwenyekiti huyo, pia, alipata nafasi ya kujionea hali ya usalama wa maghala yanayohifadhi vifaa hivyo na kuwataka maafisa wa wilaya kuhakikisha yanakuwa salama muda wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *