
Jukwaa la 5 la Biashara na Uchumi kati ya Uturuki na Afrika (TABEF) limehitimishwa Ijumaa mjini Istanbul, likidumisha moja ya ushirikiano unaokua kwa kasi zaidi kati ya nchi za Kusini mwa dunia.
Kwa kauli mbiu ya: “Kuhamasisha Mahusiano ya Uturuki na Afrika kwa Manufaa ya Pande Zote”, jukwaa hili lilikutanisha zaidi ya washiriki 4,000 wakiwemo wakuu wa nchi, mawaziri, mabalozi na viongozi wa sekta binafsi kutoka barani Afrika na Uturuki.
Katika hotuba yake kuu iliyosubiriwa kwa hamu, Kamishna Belobe alieleza kuwa ushirikiano wa Uturuki na Afrika “siyo tu halisi, bali hauwezi kurudishwa nyuma.”
Kauli hiyo inaonyesha makubaliano yanayokua miongoni mwa viongozi kuwa ushirikiano huu hauko tena katika hatua ya kuanza, bali tayari umejengeka na unabadilisha namna nchi zinazoenedela kiuchumi zinavyofanya biashara.
“Mshirika wa kuaminika”
“Uturuki siyo mgeni anayepita,” alisema Kamishna Belobe. “Ni mshirika wa kuaminika – anayejenga, kuwekeza, kusikiliza, na kuchukua hatua sambamba na matarajio ya Afrika.”
Kamishna huyo alionyesha ukuaji mkubwa wa kiuchumi kati ya pande hizi mbili:
“Katika kipindi kisichozidi miongo miwili, biashara kati ya Afrika na Uturuki imeongezeka kutoka dola bilioni 4.5 za Marekani mwaka 2003 hadi zaidi ya dola bilioni 40.7 mwaka 2024.”
Ukuaji huu umelifanya Uturuki kuwa miongoni mwa washirika watano wa juu wa kibiashara wasiokuwa wa Kiafrika barani humo. Kwa lengo la pamoja la kufikia dola bilioni 50 ifikapo 2026, Belobe alisema kasi ya maendeleo sio tu inaendelea – bali inazidi kuongezeka.
“Tunaona uhusiano unaoongozwa na dhamira ya kisiasa na matarajio ya sekta binafsi,” alisema. “TABEF ni ushahidi kuwa huu siyo diplomasia tu – huu ni utekelezaji.”
Ushirikiano wa zaidi ya biashara
Uwekezaji wa moja kwa moja wa Uturuki barani Afrika (FDI) sasa umepita dola bilioni 8.5, ukisaidia miradi katika nishati mbadala, miundombinu ya kidijitali, viwanda, na sekta nyingine.
Zaidi ya kampuni 1,500 za Kituruki zinafanya kazi Afrika, nyingi zikiwa na ushirikiano wa moja kwa moja na biashara ndogo na za kati (SMEs) za Kiafrika na taasisi za ndani.
“Uturuki haiwekezi ili kuchota rasilimali, bali kwa ajili ya mabadiliko,” alisisitiza Belobe. “Inasaidia biashara zetu ndogo, inashirikisha teknolojia, inajenga uwezo na inaimarisha minyororo ya thamani – huu ni mpango wa muda mrefu unaotekelezwa.”
Katika eneo la maonyesho ya jukwaa hilo, Belobe alikutana na wajasiriamali na wavumbuzi kutoka pande zote za bara.
Alieleza mfano wa kampuni ndogo ya Kiafrika inayotumia akili mnemba kubadilisha sekta ya usafirishaji, na kampuni ya Kituruki inayoshirikiana kuunda suluhisho la nishati endelevu vijijini.
“Hizi si hadithi za kusisimua tu – ni ushahidi,” alisema. “Hivi ndivyo ushirikiano wa karne ya 21 unavyopaswa kuwa – ubunifu wa pamoja, uvumbuzi na manufaa ya pande zote.”
Alisisitiza ya kwamba Afrika siyo tu wazi kwa biashara – bali inaunda mustakabali wa biashara.