Ujumbe huo umeeleza kwamba uchaguzi huo wenye utata na ambao uligubikwa na maandamano, hauzingatia kanuni za Umoja wa Afrika, mifumo ya kisheria na wajibu mwingine wa kimataifa kuhusu viwango vya uchaguzi wa kidemokrasia.

Katika ripoti yao ya baada ya uchaguzi, waangalizi hao wa Umoja wa Afrika wamesema kuwa, walishuhudia masunduku yaliyojazwa kura hata kabla ya upigaji kura kuanza katika baadhi ya vituo vya kupigiria kura, na kwamba wapiga kura walipewa zaidi ya karatasi moja ya kura na wengine waliruhusiwa kupiga kura bila uthibitisho wa utambulisho wao.

Wameongeza kwamba hakukuwepo mawakala wa vyama vya siasa katika vituo vya kura na pia wakati wa zoezi la kuhesabu kura, huku baadhi ya waangalizi walitakiwa kuondoka kwenye vituo vya kura, hali iliyozua mashaka kuhusu uadilifu wa mchakato huo.

Serikali yakanusha madai ya ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi

Licha ya madai yaliyotolewa na ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Afrika, serikali ya Tanzania imesema uchaguzi huo ulifanyika kwa njia huru, haki na uwazi.

Rais Samia Suluhu Hassan alipata ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 97 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi huo, lakini wapinzani wameituhumu serikali kwa udanganyifu.

Hata hivyo, ripoti ya waangalizi wa AU inaonekana kukinzana na ujumbe wa pongezi wa Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja huo Mahmoud Ali Youssof, aliyempongeza Samia kwa kuchaguliwa tena kuiongoza Tanzania.

Je, pongezi za Mwenyekiti huyo wa AU zinadhoofisha matokeo ya ripoti ya waangalizi wake? Barack Muluka, ni mchambuzi wa siasa nchini Kenya.

“Alistahili kama mwenyekiti wa tume ya AU kuwa mtulivu, kusuburi ripoti kamili ya AU ifikishwe kwake na pia apate ripoti kutoka kwa waangalizi wa uchaguzi na kisha baada ya hapo ndipo atoe pongezi, lakini yeye alikwenda mbio sana na kutokana na kule kwenda mbio sana kwake, ikawa sawa anaipa Umoja wa Afrika aibu.”

Rais Samia atoa wito wa mshikamano wa kitaifa

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Ujumbe wa AU ulisisitiza katika taarifa yao, “Tanzania inapaswa kutoa kipaumbele kwa mageuzi ya kisiasa na ya mfumo wa uchaguzi ili kushughulikia chanzo cha changamoto zake za kidemokrasia na za uchaguzi zilizoonekana, kabla, wakati na baada ya uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita.” 

Wakati huo huo, ripoti ya waangalizi wa SADC kuhusu uchaguzi mkuu wa Tanzania ilibaini dosari kubwa, ikiwemo vizuizi dhidi ya upinzani na madai ya kujazwa kwa masanduku ya kura katika baadhi ya vituo.

Kwa mujibu wa ripoti ya SADC, ambayo Tanzania ni mwanachama, imesema uchaguzi huo haukutimiza viwango vya kidemokrasia vinavyotakiwa na jumuiya hiyo.

Imeeleza kwamba wapiga kura wengi hawakuweza kuonyesha matakwa yao ya kidemokrasia kwa uhuru, hasa kutokana na mazingira ya vitisho na ukosefu wa uwazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *