
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, anasema Marekani lazima ikabiliane na matokeo ya kisheria na kisiasa ya kitendo chake cha uchokozi mbaya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, mapema mwaka huu.
Ametoa matamshi hayo wakati wa kikao cha wazi cha Bunge leo Jumapili, siku tatu baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kukiri kwamba “ndiye aliyehusika sana” na mashambulio haramu ya mwezi June ya Israel na Marekani dhidi ya Iran.
“Kufuatia kukiri waziwazi kwa rais wa Marekani kwamba alihusika pakubwa na moja kwa moja katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran—ambao ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, Mkataba wa Umoja wa Mataifa na mmlaka yetu ya kitaifa—mimi, kwa niaba ya watu watukufu na wenye heshima wa Iran, nalaani vikali kitendo hicho kiovu,” amesema Qalibaf.
Amesema: “Ninatangaza kwamba, chini ya sheria za kimataifa, serikali ya Marekani lazima ikubali matokeo ya kisheria, kisiasa na kijeshi ya uchokozi huo wa wazi, ambao umesababisha mauaji ya raia wetu wengi.”
Qalibaf pia ameonya kwamba taifa la Iran linasimama kwa umoja na imara dhidi ya tishio lolote, na kwamba litawawajibisha wavamizi kwa matendo yao.
Israel, ikisidiwa na Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi, ilianzisha mashambulizi yasio na sababu dhidi ya Iran mnamo Juni 13, katika vita vya siku 12 vilivyoua watu wasiopungua 1,064, wakiwemo makamanda waijeshi, wanasayansi wa nyuklia na raia wa kawaida.
Marekani pia iliingia vitani kwa kushambulia maeneo matatu ya nyuklia ya Iran. Vikosi vya Jeshi la Iran vilijibu mashambulizi hayo kwa kulenga maeneo ya kimkakati katika maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu ya Palestina pamoja na kambi ya anga ya jeshi la Marekani ya Al-Udeid huko Qatar, ambayo ndiyo kambi kubwa zaidi ya kijeshi ya Marekani, Asia Magharibi.