Waziri wa vita wa utawala wa kizayuni wa Israel, Yisrael Katz amemshambulia kwa matusi makali Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan baada ya mahakama ya nchi hiyo kutoa hati za kukamatwa viongozi 37 wa utawala huo ghasibu kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya kimbari ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.

Kwa mujibu wa chaneli ya Russial-Youm, Katz ameeleza katika maandiko mawili yaliyochapishwa kwa Kituruki na Kiebrania kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii X kumhutubu rais wa Uturuki: “Erdogan, chukua hati zako za kipuuzi za utiaji nguvuni na tokomea. Hati hizi zinafaa zaidi kwa uhalifu uliofanya wewe dhidi ya Wakurdi. Israel ina nguvu na haiogopi chochote”.

Waziri wa vita wa utawala wa kizayuni ameashiria pia katika andiko lake hilo upinzani wa Tel Aviv kwa ushiriki wa askari wa Uturuki katika Kikosi cha Kimataifa cha kuleta uthabiti huko Ghaza na kumhutubu Erdogan: “wewe unaweza kuiona Ghaza kwa darubini tu”.

Ijumaa ya tarehe 8 Novemba, ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa Istanbul ilitoa hati za kukamatwa viongozi na maafisa 37 wa utawala wa kizayuni wa Israel kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji ya kimbari yaliyofanywa kwenye Ukanda wa Ghaza.

Viongozi hao wa kizayuni ni pamoja na waziri mkuu Benjamin Netanyahu, waziri wa vita Israel Katz, waziri wa usalama wa taifa Itamar Ben-Gvir, mkuu wa jeshi Eyal Zamir, na kamanda wa vikosi vya wanamaji vya Israel David Saar Salama.

Wazayuni hao wamepigwa marufuku kuingia ndani ya ardhi ya Uturuki na kupita kwenye anga ya nchi hiyo.

Itakumbukwa kuwa mnamo Novemba 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC ilitoa hati ya kukamatwa Netanyahu na waziri wa zamani wa vita wa utawala wa kizayuni Yoav Gallant kwa kuhusika na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanywa dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.

Hadi sasa utawala ghasibu wa Israel umeshawaua shahidi zaidi ya Wapalestina 69,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuwajeruhi wengine zaidi ya 170,000 katika vita vya kinyama na mauaji ya kimbari uliyoanzisha huko Ghaza Oktoba 2023…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *