
Msemaji wa Ikulu ya Russia, Kremlin Dmitry Peskov amesema, nchi hiyo haina nia ya kukiuka majukumu yake chini ya makubaliano ya kimataifa yanayopiga marufuku majaribio ya nyuklia, lakini itachukua hatua ya kuanza tena kufanya majaribio hayo ikiwa nchi zingine zitafanya hivyo,
Peskov ametoa kauli hiyo kama mjibizo kwa utatanishi uliochochewa na agizo lililotolewa wiki iliyopita na Rais wa Marekani Donald Trump kwa wizara ya vita ya nchi hiyo Pentagon la kujiandaa kuanza tena majaribio ya nyuklia. Trump alizituhumu Russia na China kuwa zinafanya majaribio ya nyuklia “kwa siri”, dai ambalo nchi zote hizo mbili zimelipuuza na kulitoa maanani.
Kufuatia matamshi hayo ya Trump, Rais Vladimir Putin wa Russia alithibitisha tena msimamo wa nchi yake wa kufungamana na Mkataba wa Marufuku Kamili ya Majaribio ya Nyuklia unaotambuliwa kimataifa, lakini akaonya kwamba ikiwa Marekani au wengineo wataanza tena kufanya majaribio, Moscow itachukua “hatua zinazofaa za kujibu mapigo.” Baadhi ya vyombo vya habari vya Magharibi vilitafsiri kimakosa matamshi yake kwa kulichukulia kama agizo la kujiandaa kwa ajili ya kufanya majaribio hayo.
Katika mahojiano aliyofanyiwa na mwandishi wa habari Pavel Zarubin yaliyorushwa hewani jana Jumapili, msemaji wa Kremlin alisema: “ikiwa nchi nyingine itafanya hivi, tutalazimika kufanya hivyo ili kudumisha hali ya mlingano,” na akasisitiza juu ya alichokiita mlingano wa kinyuklia kuwa ni “moja ya vipengele muhimu zaidi vya usanifu wa usalama wa kimataifa.”
Aidha, Peskov ametoa maanani wasiwasi ulioonyeshwa na Magharibi kuhusu majaribio ya hivi karibuni yaliyofanywa na Russia ya kombora la kruzi la Burevestnik linalotumia nguvu za nyuklia na ndege isiyo na rubani ya chini ya maji ya Poseidon ambayo yalifanywa kabla ya tangazo la Trump, akisema kwamba hakuna hata moja kati ya majaribio mawili hayo liliohusisha miripuko ya nyuklia.
Hapo awali, Makamu wa Rais wa Marekani J.D. Vance alilielezea agizo lililotolewa na Trump la kufanya majaribio ya nyuklia kama njia ya kuhakikisha silaha hizo za Washington zingali “zinafanya kazi vizuri”…/