India. Mke wa mwigizaji na mtayarishaji mkongwe wa filamu za Bollywood, Sanjay Khan, Zarine Khan, aliyefariki dunia Novemba 7, 2025 kutokana na shambulio la moyo (cardiac arrest) akiwa na umri wa miaka 81, ameacha gumzo siku ya mazishi yake.

Mazishi yake yalifanyika siku hiyohiyo jijini Mumbai nchini India yakihudhuriwa na marafiki wengi wa karibu wa familia kutoka tasnia ya filamu.

Kwenye mazishi ya mwanamama huyo, kulizuka gumzo hasa mitandaoni kuwa kwa nini Zarine alizikwa kwa taratibu za Kihindu ilihali aliolewa ndoa ya Kiislamu.

KWA NINI ALIZIKWA KIHINDU?

Ni swali lililokuwa likiulizwa na baadhi ya mashabiki wengi kwa nini mazishi ya Zarine yalifanyika kwa desturi za Kihindu badala ya zile za Kiislamu, ilhali familia ya Khan inafahamika kuwa ya Kiislamu.

Katika video zilizozagaa mtandaoni, ilionekana Zayed Khan ambaye ni mtoto wao aliongoza ibada ya mazishi chini ya uongozi wa pandit (mtaalamu wa dini ya Kihindu), huku wajukuu wa Zarine wakibeba mwili wake.

Kwa mujibu wa ripoti kadhaa za vyombo vya habari vya India, hatua hiyo ilichukuliwa ili kutimiza wosia wa mwisho wa Zarine ambaye alitaka kufanyiwa ‘dah-sanskaar’ yaani maziko ya mwili kwa moto kwa mujibu wa mila za Kihindu.

Inasemekana kuwa, Zarine kabla ya ndoa alizaliwa Mhindukike kwa jina Zarine Katrak na hakuwahi kubadili dini alipofunga ndoa na Sanjay Khan.

Hata hivyo, katika mahojiano ya zamani Zarine mwenyewe alisema kuwa alikuwa Mzooroastria (Zoroastrian) dini inayofuatwa na jamii ya Parsi.

“Sisi tulikuwa tofauti kabisa. Yeye (Sanjay) alikuwa mtu mtulivu, alivaa shati jeupe, suruali na makobazi ya Kolhapuri, akiwa na kitabu cha Tolstoy mkononi, mimi nilikuwa msichana wa kisasa wa Kizoroastria, navaa sketi na viatu vya muziki wa rock and roll.”

Kwa hiyo kila kilichofanyika kwenye mazishi yake ilitokana na wosia na dini ya mwanamama huyo aliyedumu muda mrefu kwenye ndoa na Sanjay.

MAZISHI YA WAZOROASTRIA

Kulingana na tamaduni za dini ya Zoroastria, njia ya jadi ya kuaga marehemu inajulikana kama Dokhmenashini. Katika utaratibu huo mwili wa marehemu huwekwa ndani ya ‘Tower of Silence’ jengo la duara lililo wazi juu ambapo mwili huachwa wazi kwenye jua.

Ndege kama tai, kunguru na tai mkubwa hula mabaki ya mwili huo, jambo linaloashiria kurudi kwa mwili katika asili ya dunia.

Hata hivyo, kutokana na kupungua kwa idadi ya ndege hao nchini India, jamii nyingi za Wazoroastria siku hizi huchagua njia mbadala ya kuchomwa moto.

Hata mwili wa mfanyabiashara maarufu, Ratan Tata ulifanyiwa maziko kwa njia hiyo katika krematorium ya Mumbai, ikiwa ni ishara ya mabadiliko ya desturi hizo za zamani.

HISTORIA YA PENZI LAO

“Nilipokutana na Zarine nilijua ndiye mwanamke niliyetaka kumuoa. Nilihisi faraja kwake, nilifurahia kumtazama, macho yake yalikuwa mazuri, alikuwa na tabasamu lenye kuvutia na mwili wa kupendeza, alikuwa mrembo sana,” alisema Sanjay kwenye moja ya mahojiano

Kabla ya ndoa yao, Zarine Katrak alikuwa mwanamitindo maarufu katika miaka ya 1960. Pia aliwahi kuigiza kwenye filamu kama Tere Ghar Ke Saamne na Ek Phool Do Mali, akipata umaarufu mkubwa kwa mvuto na uigizaji wake wa kipekee.

Baada ya kuolewa na Sanjay Khan, Zarine alijitoa kwenye uigizaji na kujikita kwenye usanifu wa nyumba na mapambo ya ndani (interior design). Alitumia ubunifu wake pia katika uandishi, akichapisha vitabu vya mapishi na makala kuhusu mtindo wa maisha.

Zarine Khan anakumbukwa sio tu kama mke na mama mwenye upendo, bali pia kama msanii mwenye kipaji, mbunifu mahiri na mwanamke aliyechangia kwa kiasi kikubwa katika ulimwengu wa sanaa na urembo nchini India.

Wawili hao wamebarikiwa watoto wanne Sussanne Khan, Zayed Khan, Farah Ali Khan, na Simone Khan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *