Gazeti la The New York Times la nchini Marekani limetahadharisha kwamba ikiwa Israel itaishambulia tena Iran, Tehran itajibu hujuma hiyo kwa nguvu zaidi, kwa kurusha makombora 2,000 kwa wakati mmoja kuulenga utawala huo wa kizayuni.

Katika ripoti yake inayochunguza hali ilivyo hivi sasa kati ya Iran na utawala wa Kizayuni, gazeti hilo linalochapishwa nchini Marekani limeandika: “bila kuwepo mazungumzo, bila kuwepo uangalizi na bila kuwepo uwazi kuhusu kiwango cha akiba ya nyuklia ya Iran, wengi katika eneo wana wasiwasi kwamba kutokea vita vingine kati ya Iran na Israel ni jambo lisiloepukika na kwamba kujiri kwa vita hivyo ni suala la muda tu”.

New York Times limeendelea kueleza katika ripoti yake: “ingawa Rais wa Marekani Donald Trump ametamka mara kadhaa kwamba ameangamiza uwezo wa Iran wa kurutubishaji urani, lakini wataalamu na wachambuzi wametilia shaka dai hili.”

Gazeti hilo limemnukuu mkurugenzi wa mradi wa Iran katika “Jopo la Kimataifa la Migogoro” akisema: “ikiwa Israel itashambulia tena Iran, jibu la Tehran litakuwa kali zaidi kuliko la mwezi Juni.”

New York Times limeongezea kwa kusema: “viongozi wa Iran wamesema, viwanda vya makombora vinafanya kazi kutwa kucha na kwamba endapo vita vingine vitatokea, Iran imedhamiria kurusha makombora elfu mbili kwa mpigo ili kusambaratisha mitambo ya ulinzi ya Israel, na si makombora mia tano tu kwa muda wa siku 12 kama ilivyokuwa katika vita vilivyopita”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *