Kundi la kutetea haki za waandishi wa habari wa Palestina limeripoti kuwa jeshi la Israel limewaua waandishi wa habari 44 wa Palestina katika mahema ya wakimbizi huko Gaza, wakiwa kati ya zaidi ya wafanyakazi 270 wa vyombo vya habari waliouawa na utawala huo katika eneo linalozingirwa la Ukkanda wa tangu Oktoba 2023.

Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na Freedoms Committee of the Palestinian Journalists Syndicate, mahema ya waandishi wa habari karibu na hospitali na makazi yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa yalipigwa mabomu, na makazi ya wakimbizi yalilengwa moja kwa moja na wanajeshi wa Israel.

Ripoti hiyo imeangazia mashambulizi ya makusidi yanayofanywa na Israel dhidi ya sekta ya vyombo vya habari vya Palestina na miundombinu yake.

Mashambulizi hayo yanajumuisha uharibifu wa ofisi na taasisi za vyombo vya habari, pamoja na kuwashambulia waandishi wa habari moja kwa moja katika nyumba na vyumba vyao vya kulala.

Zaidi ya hayo, waandishi wa habari wameuawa ndani ya makazi ya muda waliyolazimika kutumia baada ya kuhamishwa kwenye nyumba zao kwa nguvu.

Imesisitiza kwamba kuwalenga waandishi wa habari raia ni uhalifu wa kivita chini ya Kifungu cha 79 cha Itifaki ya Kwanza ya Ziada ya Mikataba ya Geneva.

Vilevile, mashambulizi dhidi ya mahema ya wakimbizi yaliyo karibu na hospitali na shule yametajwa kuwa ni ukiukaji mkubwa wa kinga inayotolewa kwa maeneo kama haya kibinadamu.

Ripoti hiyo pia imetoa wito wa kuimarishwa hatua za ulinzi, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa njia salama za kuingilia na maeneo salama kwa ajili ya waandishi wa habari.

Mapema mwezi Agosti, waandishi sita wa habari, akiwemo Anas al-Sharif wa Al Jazeera, waliuawa katika shambulio la anga la Israel dhidi ya wafanyakazi wa vyombo vya habari waliokuwa wamekimbilia hifadhi kwenye hema nje ya lango kuu la Hospitali ya al-Shifa ya Jiji la Gaza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *