Mtandao wa Madaktari wa Sudan umeripoti kuwa, maiti za mamia ya raia zimezikwa katika makaburi ya pamoja na nyingine zimechomwa moto na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) mjini El-Fasher magharibi mwa nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na mtandao huo imesema: “Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) vimekusanya mamia ya miili kutoka mitaani na vitongoji vya mji, na kuzizika baadhi yao katika makaburi ya pamoja na kuzichoma moto zingine katika jaribio la kuficha ushahidi wa uhalifu wao dhidi ya raia”.

Mtandao huo wa Madaktari wa Sudan umeuelezea uzikaji huo wa raia hao kama “mauaji kamili ya kimbari” na “ukiukaji wa kanuni zote za kimataifa na za kidini zinazopinga ukataji wa viungo vya miili na kuhakikisha wafu wanapatiwa haki ya kufanyiwa mazishi yanayoheshimika”.

“Hali huko El-Fasher imevuka kiwango cha janga la kibinadamu na sasa imegeuka kuwa mauaji ya kimbari ya kimfumo, ikilenga uhai na heshima ya binadamu sambamba na kimya cha kusikitisha cha kimataifa ambacho kinaweza kufikia kiwango cha kuwa ushiriki (katika jinai)”, imebainisha taarifa hiyo.

“Jinai za RSF haziwezi kufutika kwa uzikaji au uchomaji moto,” imeeleza taarifa ya mtandao wa madaktari wa Sudan huku ikitoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka za kuanzisha uchunguzi huru na wa kimataifa kuhusu ukatili uliofanywa dhidi ya raia huko El-Fasher.

Mnamo tarehe 26 Oktoba, RSF ilichukua udhibiti wa El-Fasher, makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini, na kufanya mauaji ya halaiki kwa misingi ya ukabila. Hayo ni kwa mujibu wa mashirika ya ndani na ya kimataifa, huku ikitolewa tahadhari kwamba mashambulio hayo yanaweza kushadidisha hatari ya Sudan kugawanyika tena kijiografia.

Tangu tarehe 15 Aprili 2023, jeshi la Sudan, SAF na vikosi vya usaidizi wa haraka, RSF zimeingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo mazungumzo ya kikanda na ya kimataifa  yaliyofanywa hadi sasa yameshindwa kuvimaliza. Vita na mgogoro wa Sudan umesababisha vifo vya maelfu ya watu na kupelekea mamilioni ya wengine kupoteza makazi yao na kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *