Maafisa sita wa Umoja wa Ulaya walio na ufahamu wa moja kwa moja wa juhudi za utekelezaji wa awamu inayofuata ya mpango wa Trump, wamelieleza shirika la habari la Reuters kwamba mpango huo wa Trumpunaonekana kukwama na kuna uwezakano ujenzi mpya sasa kuelekezwa tu katika eneo linalodhibitiwa na Israel.

Chini ya awamu ya kwanza ya mpango huo ulioanza kutekelezwa Oktoba 10, jeshi la Israel kwa hivi sasa linadhibiti asilimia 53 ya eneo la Mediterenia, ikijumuisha kwa kiasi kikubwa mashamba, sambamba na upande wa kusini wa Rafah, sehemu ya jiji la Gaza na maeneo ya mijini.

Karibu wakaazi milioni 2 wa Gaza wameshonana katika mahema kwenye kambi na vifusi vya miji iliyoharibiwa katika maeneo yaliyosalia ya Gaza, yanayodhibitiwa na Hamas.

Rais Trump awasili Israel kulihutubia bunge la Knesset

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Awamu inayofuata inadokeza juu ya kujiondoa zaidi kwa Israel kutoka kile kinachofahamika kuwa mstari wa njano uliokubaliwa chini ya mpango wa Trump, pamoja na kuanzishwa kwa mamlaka ya mpito ya kuongoza Gaza, kupelekwa kwa kikosi cha kimataifa cha ulinzi kitakachochukua mikoba ya jeshi la Israel, kupokonywa silaha kwa kundi la Hamas na kuanza ujenzi mpya.

Lakini mpango hautoi ratiba au taratibu za utekelezaji. Wakati huo huo, Hamas inakataa kusalimisha silaha, Israel inakataa ushiriki wowote wa Mamlaka ya Palestina inayoungwa mkono na Magharibi, na kutokuwa na uhakika juu ya jeshi la kimataifa.

Mstari wa njano unachora mipaka

Vikosi vya Israel vimeweka vizuizi vikubwa vya saruji ya manjano katika mipaka ya njia ya uondoaji wanajeshi na wanajenga miundombinu upande wa Gaza unaodhibitiwa na wanajeshi wake.

Wazo moja linalojadiliwa kwa mujibu wa maafisa wawili wa Ulaya na mwanadiplomasia wa Magharibi, lilikuwa ni kama Hamas wanaweza kusalimisha silaha chini ya usimamizi wa kimataifa badala ya kuzikabidhi kwa Israel au jeshi jingine la kigeni.

Maeneo ya Palestina Jabalia 2025 | Mkokoteni wa punda katikati ya vifusi wakati wa usitishaji mapigano
Wakaazi wa Jabalia PalestinaPicha: Mahmoud Issa/REUTERS

Mataifa ya Ulaya na ya Kiarabu yanaitaka Mamlaka ya Palestina yenye makao yake makuu katika Ukingo wa Magharibi na polisi wake kurejea Gaza pamoja na jeshi la kimataifa kuchukua hatamu kutoka kwa Hamas. Maelfu ya maafisa wake waliofunzwa nchini Misri na Jordan wako tayari kupelekwa lakini Israel inapinga ushiriki wowote wa Mamlaka ya Palestina.

Ujenzi mpya chini ya ukaliaji wa Israel

Mkaazi mmoja wa Mji wa Gaza Salah Abu Amr, 62, alisema kwamba kama hakutakuwa na maendeleo yoyote katika kuwapokonya silaha Hamas na ujenzi mpya ukaanza katika mstari wa njano, watu wanaweza kufikiria kuhamia huko. Lakini uwezekano wa Gaza iliyogawika anasema ni vigumu kuufikiria.

Bado haijafahamika ni nani atafadhili ujenzi wa sehemu za Gaza chini ya ukaliaji wa Israel, huku mataifa ya Ghuba yakisita kuingilia kati bila ushiriki wa Mamlaka ya Palestina na njia ya kuwa dola, inayopingwa na Israeli. Gharama za ujenzi mpya wa Gaza zinakadiriwa kufikia dola bilioni 70.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *