Kwenye uchaguzi huo wa spika uliosimamiwa na mbunge mkongwe William Lukuvi, Zungu amewabwaga washindani wenzake watano kwa kujipatia kura 378 kati ya kura 383 na hivyo kuwa Spika wa Nane wa bunge hilo.
Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Zungu amewashukuru wabunge wote wateule kwa kuonyesha Imani kwake kumchagua yeye kuwa Spika na kwamba huo ni ushindi wa wote. Aidha Zungu ameahidi kushirikiana na viongozi wenzake wote kwa kuzingatia sheria na kanuni za bunge.
Aliongeza “Nitatoa fursa sawa kwa waheshimiwa wabunge wote, na kwamba ofisi ya spika itakuwa wazi kwa kila mbunge kwa ushauri mbalimbali.”
Hatua ya wabunge wateule kumchagua Mussa Hassan Zungu kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokelewa kwa hisia mseto katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania. Wengi wanasema huo ni uamuzi mzuri kwa kuwa wabunge hao wanamjua vyema Zungu ambaye awali alikuwa Naibu Spika.
Uzoefu unaonyesha kuwa baada ya hatua hiyo ikiwemo viapo vya wabunge wote, Spika atapokea jina moja kutoka kwa Rais, la mtu atakayependekezwa kuwa Waziri Mkuu ili apigiwe kura na wabunge na siku itakayopangwa Rais Samia Suluhu Hassan atakwenda viwanja vya Bunge kulihutubia kwa ajili ya kulizindua rasmi.