
WAAMUZI wawili kati ya watatu waliochezesha mechi ya Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), kati ya Chipukizi na New Stone, Is’haka Yona Thomas (mwamuzi wa kati) na Saleh Khalfan Mohamed (mwamuzi msaidizi namba moja), wamefungiwa miezi mitatu na kutozwa faini ya Sh500,000 kila mmoja baada ya kubainika kushindwa kuzitafsiri vizuri sheria 17 za mpira wa miguu.
Mechi hiyo iliyochezwa Novemba 9, 2025 kwenye Uwanja wa Gombani uliopo kisiwani Pemba saa 10:15 jioni, Chipukizi iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya New Stone.
Taarifa iliyotolewa leo Novemba 11, 2025 na Katibu wa Kamati ya Mashindano, Raya Sharif Nassor, imesema Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), imefanya mapitio katika ripoti ya mechi hiyo ambapo imeonesha kuwa waamuzi hao wameshindwa kuzitafsiri sheria 17 za mpira wa miguu.
Imefafanua kwamba, ripoti iliyotolewa na Kamisaa wa Mechi hiyo, imeeleza sababu kuu mbili ambazo ni kuwanyima bao halali New Stone Town kwa kushirikiana na msaidizi wake namba moja, pia kushindwa kuipa timu hiyo penalti iliyoonekana ni ya wazi.
“Ripoti ya Kamisaa imeripoti kwamba mwamuzi ameshindwa kuzitafsiri sheria 17 za mpira wa miguu huku akitaja sababu ya kuwanyima bao stahiki timu ya New Stone kwa kushirikiana na mshika kibendera namba moja na kuwanyima penalti ya wazi timu hiyo,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo, imeeleza vitendo hivyo ni kuidhalilisha New Stone na uvunjifu wa amani wa timu kwenye uwanja jambo ambalo husababisha lawama kwa wasimamizi na watendaji wa ZFF.
“Kwa mujibu wa kanuni ya kuendesha mashindano sura ya 21(9), mwamuzi I-shaka Yona Thomas na mshika kibendera Saleh Khalfan Mohamed wanafungiwa kuchezesha mechi kwa muda wa miezi mitatu na kutozwa faini ya Sh500,000 kwa kila mmoja, faini hiyo inatakiwa kulipwa Novemba 20, 2025,” imefafanua taarifa hiyo.
Tangu kuanza kwa Ligi Kuu Zanzibar msimu huu Septemba 25, 2025, hilo ni tukio la pili kwa waamuzi kufungiwa kutokana na kushindwa kuzitafsiri sheria 17 za mpira wa miguu.
Katika taarifa iliyotolewa Oktoba 6, 2025 na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi Zanzibar (ZLB), Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi ya ZLB, ilimuondoa katika ratiba mwamuzi Washington Benard kwa mizunguko mitano mfululizo kuanzia wa pili kwa kushindwa kuzitafsiri sheria hizo kwenye mchezo namba sita kati ya JKU dhidi ya KVZ.
Mechi hiyo, ilichezwa Oktoba Mosi, 2025 ikimalizika kwa sare ya mabao 2-2 ambapo ripoti ilibainisha mwamuzi huyo alikataa bao la JKU ikidaiwa mfungaji aliotea. Adhabu hiyo ilitoka kwa kuzingatia kanuni ya 3 sura 27 ya mashindano.
Mbali na hilo, baadhi ya makocha wamekuwa na malalamiko kuwa waamuzi wanachezesha ligi hiyo chini ya kiwango na wamekuwa sababu ya kuichafua.