Sharaa, ambaye wakati fulani Marekani ilimtangazia zawadi ya dola milioni 10 kwa ambaye angelifanikisha kumkamata, aliwasili kimyakimya kwenye Ikulu ya White House, akipitia mlango wa ubavuni, badala ya lango kuu la West Wing ambalo kawaida Trump huwapokelea wageni mashuhuri.

Trump alikutana na Sharaa kwenye ziara hiyo ya kwanza kabisa kwa rais huyo wa Syria mjini Washington, miezi sita baada ya mkutano wao wa kwanza nchini Saudi Arabia, ambapo kiongozi huyo wa Marekani alitangaza mipango ya kuiondoshea vikwazo Syria na siku chache tu baada ya Marekani kusema Sharaa hatambuliki tena kama “Gaidi Maalum wa Kimataifa.”

Akizungumza na waandishi wa habari, Trump alikiri kwamba maisha ya zamani ya Sharaa yalikuwa yenye utata, lakini wakati huo huo alimsifia kama “kiongozi shupavu” na akaelezea imani aliyonayo kwake.

“Tumekubaliana naye. Ni kiongozi shupavu sana. Anatokea eneo gumu kweli naye ni mtu madhubuti. Nampenda. Ninafahamiana naye, rais huyu mpya wa Syria. Na tutafanya kila tuwezalo ili Syria ifanikiwe kwa kuwa ni sehemu ya Mashariki ya Kati.” Alisema Trump.

Baadaye Sharaa alikiambia kituo cha televisheni cha Fox News kwamba uhusiano wake na kundi la wanamgambo lilikuwa jambo la zamani na halikujadiliwa kwenye mazungumzo yake na Trump. Badala yake, alisema, kwa sasa Syria inachukuliwa kama mshirika wa kilimwengu wa Washington na sio tena kitisho.

Ushirikiano na Israel?

Mbali ya masuala ya ulinzi na usalama, mazungumzo ya Trump na Sharaa yalitazamiwa pia kujikita kwenye uwezekano wa kufikia makubaliano kati ya Syria na Israel, jambo ambalo linalopiganiwa sana na utawala wa Trump, ingawa kwa upande wa Sharaa limekuwa zito sana kukubalika.

USA Washington D.C. 2025 | Donald Trump na Ahmed al-Sharaa
Rais Donald Trump wa Marekani (kushoto) akimkaribisha rais wa mpito wa Syria, Ahmed al-Sharaa, kwenye Ikulu ya White House jijini Washington siku ya Jumatatu (11 Novemba 2025).Picha: SANA/AFP

Ziara hii ya Sharaa kwenye Ikulu ya Marekani inatazamwa kama tukio kubwa kabisa kwa muasi huyo wa zamani aliyegeuka kuwa mtawala baada ya kumuangusha dikteta wa muda mrefu, Bashar al-Assad, na tangu hapo amekuwa akizuru maeneo mbalimbali duniani akijijengea taswira ya kiongozi mwenye msimamo wa wastani anayetaka kuliunganisha taifa lililosambaratishwa na vita na kukomesha miongo kadhaa ya vikwazo vya kimataifa.

Mojawapo ya malengo makubwa ya Sharaa kwenye ziara yake ya jana jijini Washington ilikuwa ni kushinikiza kuondolewa kikamilifu kwa vikwazo vyote vya Marekani.

Ingawa alikutana na Trump kwenye mkutano wa faragha, wizara ya fedha ya Marekani ilitangaza siku 180 za nyongeza kwenye usitishaji wa kile kiitwachovikwazo vya Kaizari, lakini ni Baraza la Congress pekee linaloweza kuviondosha vikwazo vyote.

Sharaa, mwenye umri wa miaka 43, aliingia madarakani mwaka jana baada ya waasi kuanzisha mashambulizi ya kushitukiza na kumuangusha Rais Assad siku chache baadaye mnamo Disemba 8. 

Tangu  hapo, Syria imejipambanuwa kusaka mwanzo mpya, ikijitenga mbali na washirika wa Assad, Iran na Urusi na ikijiegemeza zaidi kwa Uturuki, nchi za Ghuba na Marekani. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *