Katika kauli iliyotafsiriwa kama onyo lililolenga nchi jirani, Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameonya kuhusu uwezekano wa kutokea vita katika siku zijazo endapo nchi za Afrika ambazo hazina bandari zitaendelea kunyimwa haki ya kufikia Bahari ya Hindi.

Museveni ameyasema hayo katika mahojiano ya redio aliyofanyiwa mjini Mbale alipokuwa katika kampeni za uchaguzi, na akasisitiza kuwa, kuzuia nchi zisizo na bandari kufikia bahari ni “wazimu”.

Amesema, Uganda ina haki ya kutumia Bahari ya Hindi kutokana na mahitaji yake ya kiuchumi na kiusalama.

Rais wa Uganda amelalamika kuwa ni jambo lisilo la haki kuzuia nchi ambazo hazina bandari kupata njia muhimu ya biashara na ya masuala ya ulinzi wa kimkakati.

Aidha, Museveni ameelezea ugumu unaoikabili Uganda katika kuunda jeshi la wanamaji kwa ajili ya kujilinda kwa sababu haina uwezo wa kuifikia bahari.

Amesema, mara kadhaa nchi yake imekuwa na changamoto katika mazungumzo na Kenya kuhusu miradi muhimu ya miundombinu inayohitaji ufikiaji wa moja kwa moja katika Bahari ya Hindi.

Akifafanua zaidi, Museveni amesema: “hapa Uganda, hata kama tunataka kuunda jeshi la wanamaji, tunawezaje kuwa nalo bila bahari? Hatuna uwezo wa kufikia bahari. Utaratibu wa siasa za Afrika hauna mantiki. Baadhi ya nchi hazina bandari, si kwa sababu za kiuchumi tu, bali pia kwa ajili ya ulinzi. Unakwama. Tutasafirisha bidhaa zetu vipi? Ndiyo maana tumekuwa na mazungumzo na Kenya. Mazungumzo kuhusu reli, bomba la mafuta – hayaishi. Lakini ile bahari ni yangu, kwa sababu ni bahari yangu. Nina haki ya kuitumia. Na kama hali ikiendelea hivi, siku za usoni tutakuwa na vita”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *