Waziri wa masuala ya mikakati wa utawala wa Kizayuni na ambaye ni mtu wa karibu na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, amejiuzulu. Ron Dermer, ametangaza kujiuzulu kwa kumtumia barua rasmi Netanyahu.
Dermer alikuwa mtu muhimu katika baraza la mawaziri la wapenda vita na ukatili la Netanyahu na alikuwa na jukumu la kusimamia masuala nyeti, ikiwa ni pamoja na uhusiano wa utawala wa Kizayuni na Marekani, vita vya Ghaza na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Hamas. Kujiuzulu Dermer kumekuja wakati huu ambapo baraza la vita la Israel linaloongozwa na Netanyahu limekumbwa na migogoro mingi ya ndani na nje, ikiwa ni pamoja na ukosoaji mkubwa wa jinsi lilivyoshindwa kusimamia vizuri vita vya Ghaza, mashinikizo ya kimataifa na mgawanyiko wa kisiasa ndani ya utawala huo pandikizi.
Utendaji mbovu wa Netanyahu katika vita vya Ghaza unaendelea kukosolewa vikali ndani na kimataifa huku maafisa mbalimbali wa Israel wakizidisha mashinikizo na waandamanaji wakiendelea kumiminika mitaani katika maeneo mbalimbali ya ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel, wakilalamikia kushindwa baraza la vita la Netanyahu kusimamia vizuri kijeshi na kibinadamu mgogoro ulioukumba utawala wa Kizayuni hivi sasa.
Netanyahu yuko katika hali ngumu, kwani anaendelea kuelemewa na mashinikizo ya kidiplomasia kutoka hata kwa washirika wa Tel Aviv yaani madola ya Magharibi ambayo yenyewe yamelazimika kuunga mkono kukomeshwa vita vya Ghaza kutokana na shinikizo la walimwengu. Wakati huo huo, maamuzi ya mahakama ya kimataifa yametolewa dhidi ya viongozi wa Israel ambao wameburuzwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji ya kimbari na jinai za kivita.
Mashinikizo ya ndani ya baraza la mawaziri na kuendelea kupapurana vibaya Wazayuni wenye misimamo mikali ni miongoni mwa mambo mengi yaliyomuweka waziri mkuu wa Israel katika hali mbaya mno. Familia za mateka wa Israel waliokuwa wanashikiliwa na makundi ya Muqawama ya Palestina ambazo mpaka hivi sasa zimeshindwa kupata maiti za jamaa zao waliouliwa kikatili na Benjamin Netanyahu wakati wa vita vya miaka miwili huko Ghaza, hazitaki tena vita lakini Wazayuni wenye misimamo mikali katika baraza la mawaziri la Netanyahu wanashikilia kuendelea mashambulizi ya kikatili ya Israel huko Ghaza.

Kujiuzulu Ron Dermer kunaweza kusababisha ongezeko la mgogoro wa kisiasa na kiusalama ndani ya baraza la vita la Netanyahu. Kujiuzulu kwake kutaleta ombwe la kimkakati katika usimamizi wa migogoro ya usalama ya utawala wa Kizayuni. Kujiuzulu kwake ni ishara ya kuweko migogoro mikubuwa ya ndani ya utawala wa Kizayuni na kuzidi kuwa mbaya nafasi ya Netanyahu na serikali yake.
Naam tumesema kwamba kujiuzulu Ron Dermer wakati huu ambapo baraza la vita la Netanyahu limekumbwa na migogoro mingi kunaweza kuwa na athari kubwa za kisiasa na kiusalama na sababu yake ni kwamba, Dermer alikuwa mmoja wa wabunifu wakuu wa sera za usalama na kidiplomasia za Netanyahu. Kujiuzulu mtu kama yeye aliyekuwa karibu na Netanyahu huku kukiwa na maandamano ya ndani na mashinikizo ya kimataifa, ni ishara ya wazi ya kusambaratika serikali ya Netanyahu.
Kujiuzulu Dermer kumeleta pia uwezekano wa kupata nguvu ushawishi wa Wazayuni wenye misimamo mikali katika baraza la vita la Netanyahu. Magenge yenye misimamo mikali ya Kizayuni yanataka ardhi za Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan zitekwe zote na kuvunjwa kabisa utawala wa ndani wa Palestina. Si hayo tu lakini pia kujiuzulu Dermer kunaweza kuwa ni mwanzo wa kushuhudiwa wimbi la kujiuzulu viongozi wengine wa Israel, hasa kutoka kwa wajumbe wa baraza la mawaziri ambao wanazikosoa waziwazi sera za Netanyahu.
Hata vyama vya upinzani vinaamini kwamba kujiuzulu kwa Dermer ni ishara ya kuweko mgogoro ndani ya baraza la vita la Netanyahu na vinaihesabu hatua hiyo kuwa ni fursa ya kushinikiza kufanyika uchaguzi wa mapema. Wazayuni wenye misimamo mikali katika baraza la mawaziri la Netanyahu wamefurahia kujiuzulu Dermer na wanataka ateuliwe mtu katili zaidi atakayefanya mauaji makubwa zaidi dhidi ya Wapalestina na kuishambuliia tena Ghaza.
Dermer pia alikuwa na jukumu muhimu katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Hamas. Kuondoka kwake katika baraza la vita la Netanyahu kunaweza kusimamisha au kuchelewesha mchakato wa mazungumzo hayo. Matukio hayo yanaweza kuharakisha kuporomoka kisiasa Netanyahu na kama mashiniikizo ya ndani na nje yataendelea, bila ya shaka mwisho wa uongozi wa Netanyahu utakuwa mapema zaidi.