
Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limetangaza kuwa, familia tisa kati ya 10 nchini Afghanistan zinakabiliwa na njaa au zinalazimika kubeba madeni huku raia wakimbizi waliorejea hivi karibuni wakijikimu kimaisha kwa tabu katika maeneo yenye hali mbaya ya umaskini mashariki na kaskazini mwa nchi hiyo.
Ripoti ya UNDP iliyotolewa leo Jumatano imesema, Waafghani wanaorejea nchini mwao kutoka kwenye maisha ya ukimbizi wanasokotwa na hali mbaya sana ya kukosa usalama wa kiuchumi, ambapo zaidi ya nusu ya familia hizo zinasamehe huduma za matibabu ili kuweza kununua chakula, huku zaidi ya asilimia 90 miongoni mwao zikilazimika kubeba madeni.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, madeni ziliyonayo kaya hizo yanaanzia $373 hadi $900, wakati pato la wastani la kila mwezi ni $100. Hayo ni kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi ziliofanyiwa kata zaidi ya 48,000.
UNDP imeeleza katika ripoti yake hiyo, Waafghani waliorejea nchini wanajitahidi pia kupata makazi mazuri wakati kiwango cha kodi kimeongezeka mara tatu.
Ripoti hiyo imeendelea kueleza kwamba, katika wilaya za Injil na Guzara za magharibi mwa Afghanistan, “waliorejea wengi wanaishi katika mahema au majengo yaliyobomoka”.
UNDP imetoa wito wa kupatikana usaidizi wa haraka ili kuboresha hali ya maisha na huduma kwa ajili ya Waafghanistan kwenye maeneo yenye idadi kubwa ya watu hao.
Afghanistan ambayo hivi sasa inaongozwa na serikali ya muda ya Taliban, ikiwa inakabiliwa na masaibu kadhaa, yakiwemo ya kupunguziwa misaada, vikwazo na majanga ya kimaumbile yanayojirudia, likiwemo tetemeko la ardhi la mwezi Agosti lililosababisha vifo vya watu wasiopungua 2,200, inapambana kuwapokea pia raiau milioni 4.5 ambao wamerejea nchini tangu 2023.
Serikali ya Taliban imeomba msaada wa mahitaji ya kibinadamu kutoka jamii ya kimataifa baada ya tetemeko hilo la ardhi, sambamba na kulalamikia rasmi hatua ya Pakistan ya kuwafukuza kwa halaiki raia wa Afghanistan, ikisema “ina wasiwasi mkubwa” kuhusu namna Islamabad inavyoamiliana na watu hao../