
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyidd Abbas Araqchi, amefanya mazunguzmo kwa njia ya simu na mwenzake wa Uturuki Hakan Fidan, ambapo wawili hao wamejadili uhusiano wa pande mbili na matukio ya kikanda na kimataifa.
Katika mazungumzo hayo, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Uturuki, wamezungumzia uhusiano wa pande mbili, wakisisitizia umuhimu wa kuimarisha na kuendeleza uhusiano katika maeneo yote yenye maslahi kwa Tehran na Ankara.
Sambamba na kupongeza na kuthamni juhudi zilizofanywa ili kupunguza mvutano kati ya Pakistan na Afghanistan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametilia mkazo umuhimu wa kupanua mashauriano ili kulinda amani na utulivu wa kikanda na akatangaza utayari wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kusaidia katika suala hilo.
Akiashiria mfungamano uliopo kati ya amani na utulivu wa kikanda, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amesisitizia umuhimu wa kufanywa juhudi na nchi zote ili kulinda amani na utulivu katika eneo hili.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametoa salamu za rambirambi pia kufuatia vifo vya raia kadhaa wa Uturuki katika ajali ya ndege ya kijeshi na kuzifariji familia za waathiriwa…/