Timu za uokoaji za Palestina katika Ukanda wa Ghaza zimegundua na kufukua maiti zingine 51 za Wapalestina waliouliwa shahidi na jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel.

Kwa mujibu wa tovuti ya televisheni ya Al-Mayadeen, timu ya uokoaji katika Ukanda wa Ghaza imetangaza kuwa imefanikiwa kupata miili ya mashahidi hao 51 katika eneo la kandokando ya Kliniki ya Sheikh Ridhwan magharibi mwa Jiji la Ghaza.

Tangazo lililotolewa hivi karibuni na Wizara ya Afya ya Ghaza, ambalo lilichapishwa siku ya Jumanne (Novemba 10) limeeleza kwamba, jumla ya Wapalestina waliouawa shahidi katika eneo hilo la Palestina lililowekewa mzingiro imefikia 69,182. Kwa mujibu ripoti hiyo, tangu Oktoba 7, 2023 hadi sasa, Wapalestina wengine 170,694 wamejeruhiwa kutokana na vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yaliyofanywa na jeshi la utawala wa kizayuni.

Itakumbukwa kuwa, mnamo Oktoba 7, 2023, utawala wa Kizayuni ulianzisha vita dhidi ya Ukanda wa Ghaza ukiwa na malengo mawili makuu: kuiangamiza harakati ya ukombozi wa Palestina ya Hamas na kuwakomboa mateka wa kizayuni waliokuwa wakishikiliwa katika eneo hilo, lakini ulishindwa kufikia malengo hayo na ukalazimika kukubali kusitisha mapigano na kufikia mwafaka na harakati ya Hamas wa kubadilishana mateka…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *