Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza imetoa ripoti inayoonyesha kuwa, Wapalestina 6,000 wamekatwa viungo katika eneo hilo tangu utawala wa kizayuni wa Israael ulipoanzisha vita vya kinyama dhidi ya eneo hilo Oktoba 2023 na ambavyo vimeendelea kwa muda wa miaka miwili.

Ripoti hiyo imeeleza kwamba, watoto wanachangia asilimia 25 ya jumla ya watu waliokatwa viungo, na wanawake wanachangia asilimia 12.7.

Wizara ya Afya katika Ukanda wa Ghaza imesema: “uhaba wa vifaa vya matibabu na vifaa vya usaidizi unazidisha mateso ya waliojeruhiwa na waliokatwa viungo”.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, “takwimu hizo zinaonyesha mateso makubwa ya kibinadamu yanayowapata maelfu ya majeruhi na familia zao”.

Aidha, Wizara ya Afya ya Palestina imetoa wito wa kufanyika ukarabati wa haraka na utoaji huduma za usaidizi wa kisaikolojia na kijamii, hususan kwa watoto ambao sasa hivi wanakabiliwa na ulemavu wa kudumu wakiwa wangali na umri mdogo.

Utawala wa kizayuni wa Israel umeshawaua shahidi zaidi ya Wapalestina 69,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuwajeruhi wengine zaidi ya 170,600, mbali na 9,500 ambao hadi sasa hawajulikani walipo, wengi wao wakiaminika kuwa wamekwama chini ya vifusi vya nyumba zilizoharibiwa au kutokuwepo taarifa zao zozote, tangu utawala huo ghasibu ulipoanzisha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya Ghaza Oktoba 2023.

Vita hivyo vilisimamishwa chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoanza kutekelezwa tarehe 10 Oktoba kwa mujibu wa mpango wa vipengele 20 uliopendekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump.

Hata hivyo, tangu wakati huo hadi sasa, jeshi la kizayuni limeshakiuka makubaliano hayo ya kusitisha mapigano zaidi ya mara 282 na kuwaua shahidi Wapalestina wasiopungua 242 na kuwajeruhi wengine 622…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *