
Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema ukiukaji wa usitishaji vita uliofanywa Israel uliotokana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya utawala huo wa kizayuni na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu nchini Lebanon ya Hizbullah mnamo Novemba 2024 umesababisha vifo vya raia 114 wa nchi hiyo.
Msemaji wa ofisi hiyo Thameen Al-Kheetan amevieleza vyombo vya habari kuwa ofisi ya haki za binadamu inafuatilia mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel na kulenga majengo katika vijiji vya kusini na kubainisha kuwa vifo vya raia vimeendelea kuongezeka tangu ulipoanza usitishaji mapigano.
Al-Kheetan amesisitiza kuwa, athari mbaya za maafa ya roho za raia ambazo zinaendelea kushuhudiwa “lazima zikome mara moja,” na akaongeza kuwa kwa zaidi ya miaka miwili wakazi katika eneo hilo wamekuwa wakiishi kwa hofu na kukosa utulivu.
Aidha, ametoa wito wa kufungamana haraka na makubaliano hayo ya kukomesha uhasama na kuheshimiwa sheria za kimataifa za kibinadamu.
Jeshi la utawala haramu wa kizayuni wa Israel limeua zaidi ya watu 4,000 na kujeruhi karibu 17,000 katika mashambulizi yake dhidi ya Lebanon, yaliyoanza Oktoba 2023 na kugeuka vita kamili mwezi Septemba 2024…/